Katika taarifa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Hussein Jaberi Ansari amesema kuwa, "kutekelezwa hukumu ya kuuawa shakhsia kama Sheikh Nimr ambaye hakuwa na wenzo wowote isipokuwa kutumia maneno katika kufuatilia malengo yake ya kisiasa na kidini ni jambo linaloashiria upeo wa ukosefu wa busara na kutowajibika."
Ameongeza kuwa utawala wa Saudi Arabia unaunga mkono magaidi na matakfiri huku ukiwakandamiza na kuwaua wapinzani wa ndani ya nchi hiyo. Amesema Sheikh Nimr ameuawa wakati ambao magaidi wakufurishaji wamevuruga usalama na amani ya Mashariki ya Kati na dunia kwa jumla kiasi cha kutishia kuangusha baadhi ya serikali katika eneo hili. Amesema serikali ya Saudia Arabia itajuta kufuata sera kama hizo.
Mapema leo Jumamosi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa, imewanyonga watu 47 akiwemo Sheikh Nimr Baqir al-Nimr mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini humo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imedai kuwa, watu hao wamenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika operesheni za kigaidi. Hukumu ya kunyongwa wanaharakati hao imetekelezwa leo katika kitongoji cha 12 nchini humo, imebainisha taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia. Sheikh Baqir al Nimr alikamatwa na kufungwa jela na utawala wa kifalme wa Saudia mwaka 2012 akiwa katika maandamano ya kupinga dhulma za utawala huo katika eneo la Qatif lenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mahakama Kuu ya Saudi Arabia ilikuwa imepasisha hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama moja ya nchi hiyo dhidi ya mwanazuoni huyo na utekelezaji wake ulikuwa ukisubiri saini ya Mfalme Salman bin Abdulaziz. Sheikh Nimr Baqir al Nimr amekuwa akipigania uhuru na haki za binadamu hususan za Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaokandamizwa sana nchini Saudia.
Watetezi wa haki za binadamu na Waislamu kote duniani wanaendelea kuulaani vikali utawala wa kiimla wa Saudi Arabia kwa kutekeleza hukumu ya kifo ya Sheikh Nimr. Maulama wa kidini nchini Iran pia wamelaani vikali hukumu hiyo huku maandamano makubwa yakipangwa kufanyika kote nchini katika siku zijazo kulaani hukumu hiyo ya kidhalimu.