Habari zinasema kuwa, shambulio hilo la jana Jumatatu limetokea katika kijiji cha Nguetchewe, eneo la kaskazini, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria. Walioshuhudia hujuma hiyo wanasema kuwa, walimuona kijana barobaro ambaye walishuku mienendo yake kabla ya yeye kuingia msikitini hapo na kujiripua. Hakuna kundi lolote la kigaidi lililokiri kuhusika kwenye hujuma hiyo ingawa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limekuwa likitekeleza mashambulizi ya aina hii nchini Cameroon. Wiki iliyopita, watu wasiopungua 13 waliuawa baada ya kutokea shambulio la bomu katika msikiti mwingine, katika eneo la Kolofata kaskazini mwa Cameroon.
Kwa muda wa miaka sita sasa, kundi la Boko Haram linafanya
mashambulizi dhidi ya Waislamu na Wakristo na taasisi za serikali katika nchi
za eneo la Magharibi mwa bara Afrika. Zaidi ya watu 20 elfu wameshauwa, mamia
ya maelfu ya wengine kujeruhiwa na wengine wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya
eneo hilo kutokana na mashambulizi ya Boko Haram.