IQNA

Dkt. Velayati

Wakufurishaji wameibuliwa kuvuruga mwamko wa Kiislamu

14:44 - January 30, 2016
Habari ID: 3470100
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesema lengo kuu la kuibuliwa makundi ya wakufurishaji wa Kiwahhabi ni kukabiliana na wimbi la mwamko wa Kiislamu.

Dkt. Ali Akbar Velayati ameyasema hayo katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Hatari ya Makundi Yanayowakufurisha Waislamu uliofanyika Jumatano na Alhamisi katika mji wa Qom nchini Iran. Velayati amesema mwamko wa Kiislamu uliana mapema karne ya 19 kwa lengo la kukabiliana na wimbi la hujuma ya Wamagharibi katika nchi za Kiislamu.

Amesema wimbi la pili la Mwamko wa Kiislamu lilianza kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran mwaka 1979 ambapo baada ya hapo madola kama vile Uingereza, Marekani na Saudi Arabia zilishirkiana katika kuunda kundi la kigaidi la al Qaeda na kisha makundi kama ISIS au Daesh ili kukabiliana na mrengo wa mapambano au muqawama ulio dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo.

Velayati amebaini kuwa miongoni ma malengo ya kuanzisha na kuyasaidia makundi ya kigaidi na kitakfiri huko Syria ni kukata uhusiano baina ya Iran na Palestina na kudhamini usalama wa Israel. Ameashiria njama za maadui wa Uislamu za kupotosha malengo ya mwamko wa Kiislamu katika nchi mbalimbali na kusema: Maadui wanafanya mikakati ya kuanzisha Uislamu mbadala ambao dhihirisho lake ni makundi ya kitakfiri kama lile la ISIS katika nchi za Syria na Iraq na kabla yake makundi ya al Qaida na Taliban.

Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Hatari ya Makundi Yanayowakufurisha Waislamu ulifanyika kwa lengo la kuanzisha umoja na mshikamano baina ya maulama wa Kiislamu kwa ajili ya kuunda muungano wa kukabiliana na makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine na kuamsha hisi ya kuwajibika baina ya maulama na wanazuoni wa Kiislamu. Mkutano huo umehudhuriwa na mamia ya maulama wa madhehebu za Shia na Suni kutoka nchi mbalimbali. Taarifa ya mwisho ya mkutano huo imeashiria hali mbaya ya sasa katika nchi za Waislamu na kusema: Harakati zinazozusha mifarakano za makundi yanayowakufurisha Waislamu zimesababisha mauaji, ukatili, vita vya kimadhehebu, kuwaweka Waislamu mbali na masuala yao muhimu na kuimarisha kambi ya maadui wa Uislamu; katika mazingira hayo ni wajibu kwa wanazuoni na maulama wa Kiislamu kuyapiga vita makundi hayo na kuarifisha sura halisi ya Uislamu.

Taarifa ya Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Hatari ya Matakfiri imesema kuwa, maadui wa dini tukufu ya Uislamu wanayatumia makundi hayo kwa shabaha ya kupeleka mbele malengo yao katika nchi za Waislamu na kuzuia kuenea zaidi dini hiyo duniani kupitia mradi wa propaganda na kuchafua sura ya Uislamu; kwa msingi huo maulama wametakiwa kutekeleza vyema majukumu yao ya kuwazindua Waislamu kuhusu njama hizo. Vilevile imetilia mkazo udharura wa kutatuliwa hitilafu zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu kwa kutumia njia ya mazungumzo.

Mkuu wa Sekretarieti ya Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Hatari ya Makundi ya Kitakfiri, Hujjatul Islam Abdul Majiid Hakiim-Ilahi amesema katika hotuba ya kufunga mkutano huo kwamba, maadui wa Uislamu wanatumia stratijia ya kuanzisha vita baina ya Waislamu kupitia njia ya kuasisi makundi ya kitakfiri na yenye misimamo ya kuchupa mipaka yanayofanya kazi ya kuchafua sura halisi ya Uislamu na kuzusha hitilafu na fitina baina ya wafuasi wa dini hii tukufu.

3470951

captcha