IQNA

Kiongozi Muadhamu: Iran itampigisha magoti adui kwa Uwezo wa Mwenyezi Mungu

20:11 - January 03, 2026
Habari ID: 3481757
IQNA – Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kusimama pamoja na wananchi “Inshaallah, tutampigisha magoti adui.”

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo Jumamosi jijini Tehran katika kikao na familia za mashahidi, ikiwemo familia ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyeuawa shahidi na jeshi la Marekani mjini Baghdad, Iraq, tarehe 3 Januari 2020.

Akashiria machafuko ya hivi karibuni Iran yaliyoanza katika Bazaar au Soko Kuu la Tehran wiki iliyopita, Ayatullah Khamenei alisema tabaka la wenye maduka katika bazaar ni “miongoni mwa tabaka la waaminifu zaidi kwa Mapinduzi ya Kiislamu,” akisisitiza kuwa “haiwezekani kupambana na mfumo wa Kiislamu kwa kisingizio cha soko na wafanyabiashara.”

Amesema kuwa malalamiko ya wafanyabiashara yana msingi, kwani mfanyabiashara anapoangalia hali ya fedha, kushuka kwa thamani ya sarafu ya taifa na kuyumba kwake, “husema, ‘siwezi kufanya biashara,’ na hili ni kweli.”

Ayatullah Khamenei aliongeza kuwa rais na viongozi wakuu wanatafuta tiba ya hali hiyo, akibainisha kuwa kupanda kwa thamani ya fedha za kigeni bila udhibiti ni jambo lisilo la kawaida na lina “mkono wa adui,” ambao lazima ukomeshwe.

Kiongozi Muadhamu alionya dhidi ya kutumia malalamiko halali ya kiuchumi kwa maslahi ya maadui, na kuongeza kuwa kilicho muhimu ni kwamba “baadhi ya watu waliochochewa, ambao ni vibaraka wa adui, wanasimama wenye maduka katika bazaar na kupaza kauli dhidi ya Uislamu, dhidi ya Iran na dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.”

Ayatullah Khamenei alisisitiza kuwa “maandamano ni halali, lakini maandamano ni kitu tofauti na vurugu,” akiongeza kuwa viongozi wanapaswa kuzungumza na waandamanaji, kwa sababu “mazungumzo na mwandamanaji ni tofauti na mazungumzo na mhalifu wa vurugu; kuzungumza na mhalifu wa vurugu hakufai, na mhalifu wa vurugu lazima aonyeshwe mahali pake.”

Amesema kuwa “hakubaliki kabisa” kwa makundi kuja “kwa majina mbalimbali kwa nia ya uharibifu na kuleta machafuko,” kisha kusimama nyuma ya “wenye maduka katika bazaar ambao ni waaminifu, wenye fikra salama na wenye roho ya mapinduzi,” na kutumia malalamiko yao kuanzisha fujo.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza umuhimu wa kutambua mbinu za adui, akisema adui “haketi bure bali hutumia kila fursa,” na kuongeza kuwa viongozi wapo na wataendelea kuwepo katika uwanja wa matukio, lakini “kilicho muhimu ni umoja wa taifa zima.”

Ayatullah Khamenei amesema kuwa pale adui anapojaribu kulazimisha matakwa yake kwa kiburi dhidi ya nchi, serikali na taifa, ni lazima “kusimama imara mbele ya adui na kufunua kifua cha uthabiti.”

“Hatutarudi nyuma mbele ya adui, na kwa kutegemea Mwenyezi Mungu na msaada wa wananchi, Inshaallah, tutampigisha magoto adui.”

Sifa za Shahidi Qassem Soleimani

Kiongozi Muadhamu katika sehemu nyingine ya hotuba yake alifafanua zaidi kuhusu sifa za kipekee za Shahidi Qassem Soleimani, akisema kuwa mambo matatu,  imani, ikhlasi na utendaji, ndiyo yalikuwa mhimili wa utu wa shahidi huyo, ambaye alimuelezea kama “mwanadamu kamili wa zama zetu.”

Ayatullah Khamenei alionyesha imani ya kina ya Jenerali Soleimani kwa Mwenyezi Mungu, msaada wa ghaibu na usahihi wa njia aliyokuwa akiifuata.

Akasema kuwa Shahidi Soleimani alikuwa “mtu mwenye ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu ,” ambaye hakutenda kwa ajili ya sifa, umaarufu au makofi ya watu, bali kwa wajibu na utiifu.

Akimsifu kwa uwepo wake wa kudumu katika kila uwanja uliokuwa ukihitajika, Kiongozi Muadhamu alisema Jenerali Soleimani alisimama kinyume na wale “wanaoelewa vizuri na kusema vizuri, lakini hawachukua hatua.”

Ayatullah Khamenei alibainisha kuwa Jenerali Soleimani alichukua jukumu muhimu katika kulinda na kuelekeza mwelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu, kupambana na njama za kuvuruga utulivu huko Kerman, na baadaye katika Kikosi cha Quds.

Ametaja pia mchango wake katika kulinda makaburi matakatifu, kupambana na kundi la kigaidi la Daesh, na kutekeleza majukumu katika nyanja nyingine muhimu.

Kiongozi Muadhamu alisisitiza kuwa urithi wa Jenerali Soleimani haukuwa tu katika mikakati yake, bali katika umoja wa imani, usafi wa nia na utayari wa kuchukua hatua vilivyotawala maisha na mwenendo wake.

3495945

captcha