IQNA

Wanaharakati wa Palestina wamsifu Meya Mamdani wa New York kwa hatua dhidi ya Israel

20:46 - January 03, 2026
Habari ID: 3481760
IQNA-Wanaharakati wa kutetea haki za Wapalestina wamemsifu Meya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, kwa kufuta amri za kiutawala zilizokuwa zikizuia shughuli za makundi yanayounga mkono Palestina.

Ndani ya saa chache baada ya hafla yake ya kuapishwa Jumatano, muda mfupi kabla ya usiku wa manane, na katika siku yake ya kwanza rasmi ofisini Alhamisi, Mamdani alifuta amri zote za kiutendaji zilizotiwa saini na mtangulizi wake, Eric Adams, baada ya Septemba 26, 2024, siku ambayo Adams alishtakiwa kwa rushwa na kupokea michango haramu ya kampeni kutoka vyanzo vya kigeni.

Adams alitia saini amri hizo za  kuunga mkono utawala haramu wa Israel chini ya mwezi mmoja uliopita, hatua iliyotafsiriwa kama jaribio la kumuwekea vizingiti Mamdani, ambaye ana umri wa miaka 34.

Adams pia alikabiliwa na mashtaka ya njama, ulaghai wa mawasiliano, na rushwa. Mwanasiasa huyo wa miaka 64, aliyewahi kuwa afisa wa polisi, alishtumiwa kufanya upendeleo kwa wafanyabiashara wa kigeni kwa kubadilishana na safari za kifahari na manufaa ya usafiri wa anga.

Mkurugenzi wa tawi la New York la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), Afaf Nasher, alimsifu Meya Mamdani kwa kufuta amri iliyokuwa ikizuia uwezo wa wakaazi wa New York kukosoa, kususia, na kuandaa maandamano dhidi ya utawala wa Israel kwa sababu ya ubaguzi unaoendelea na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina, pamoja na vita vya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi wa Kipalestina-Mmarekani, YL Al‑Sheikh, pia alimpongeza Meya Mamdani kwa kufuta amri hizo.

“Nadhani ni jambo la kupendeza kwamba Meya Mamdani alichukua hatua siku ya kwanza kuimarisha haki zetu za uhuru wa kujieleza, ikiwemo haki yetu ya kukosoa na kupinga ubaguzi wa Israel na mauaji ya halaiki,” alisema Al‑Sheikh.

Aliongeza kuwa amri zilizopitishwa na Adams “hazikuhusu kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi, bali zililenga kunyamazisha upinzani, jambo ambalo Wamarekani wote wanapaswa kulikataa.”

Nasreen Issa, mwanachama wa Harakati ya Vijana wa Palestina jijini New York, alisema, “Uamuzi wa Mamdani kuzikataa amri hizi ni hatua chanya katika kulinda haki za wakaazi wa New York na hadhi ya Wapalestina.”

Meya Mamdani ndiye Meya wa kwanza wa jiji hilo kuwa Mwislamu, wa kwanza kutoka Asia ya Kusini, wa kwanza kuzaliwa barani Afrika, na wa kwanza kuapishwa kwa kutumia Kitabu Kitukufu cha Kiislamu, Qur’ani.

Hafla ya kuapishwa ilifanyika Jumatano, muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mwaka Mpya 2026, katika kituo cha zamani cha reli ya chini ya ardhi cha City Hall, kilichopo chini ya Lower Manhattan.

/3495943

captcha