Rais wa Somalia ameiambia televisheni ya al Jazeera ya Qatar kwamba hatua ya Tel Aviv ya kulitambua eneo la Somaliland haikutarajiwa na ni ya kushangaza. Amesema, Israel ni utawala wa kwanza kuitambua Somaliland kama taifa huru tangu mwaka 1991.
Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe lakini haijawahi kutambuliwa rasmi na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.
Mogadishu imepinga madai hayo ya kuwa taifa huru Somaliland na kusema kuwa eneo hilo ni sehemu ya Somalia.

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amesema kuwa wamekuwa wakifanya jitihada za kuliunganisha taifa kwa njia ya amani.
Amesema, Somaliland pia imekubali kujiunga na 'Mkataba wa Abraham' uliosainiwa mwaka 2020 kati ya Israel na Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco ili kuhuisha uhusiano.
"Utawala wa Israel unataka kudhibiti njia za kimkakati za baharini za Pembe ya Afrika na kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Ghaza na kuwapeleka Somaliland.
Mataifa na asasi mbalimbali za Kiafrika, Kiarabu na Kiislamu zimepinga vikali hatua ya utawala vamizi wa Israel ya kulitambua rasmi eneo la 'Somaliland', ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili, hatua ambayo imekabiliwa na radiamali kali ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa.
Upinzani huo ni mkubwa kiasi kwamba, umeitambua hatua ya Israel kuwa, inakiuka wazi sheria za kimataifa na ni tishio kubwa dhidi ya usalama na uthabiti wa eneo la Pembe ya Afrika.
Kijiografia Somaliland iko kaskazini mwa Somalia mashariki mwa bara la Afrika, kwenye pwani ya kusini ya Ghuba ya Aden. Eneo hilo linapakana na Djibouti kwa upande wa kaskazini magharibi na Ethiopia kwa upande wa kusini magharibi huku likipakana na Somalia kwa upande wa mashariki.
4326256