
Michel Salim Kaadi, mwandishi na mshairi Mkristo wa Lebanon aliyezaliwa mwaka 1944, ni miongoni mwa watu mashuhuri katika ulimwengu wa Kiarabu waliotoa maisha yao ya kifikra kuandika na kueneza fikra za Ahlul-Bayt wa Mtume Muhammad (SAW). Kama Mkristo, Kaadi anawaona Ahlul-Bayt au watu wa nyumba ya Mtume Muhamamd (SAW) kuwa ni watakatifu na wateule wa Mwenyezi Mungu, na ameandika vitabu vyenye maudhui ya kiroho kuhusu Imam Ali (AS) na Bibi Fatima Zahra (SA).
Mtazamo huu wa kipekee umemfanya aheshimiwe na Waislamu na Wakristo, na maandiko yake yanatambulika kama mfano bora wa mazungumzo ya kidini na kukaribiana kwa fikra.
Mbali na kuzingatia Ahlul-Bayt na shakhsia wengine Kiislamu, Kaadi akiwa Mkristo wa dhati ana mtazamo wa kipekee kuhusu Nabii Isa (AS) na mafundisho ya Ukristo yanayozidi mipaka ya teolojia pekee. Fikra zake juu ya Ukristo zinajengwa juu ya utakatifu na zuhudi, akimwona Isa (AS) si tu kama nabii bali pia kama mfano wa juu wa tasawwuf na utakatifu, mtazamo unaoshirikiana na heshima yake kwa watakatifu wa Kiislamu. Katika maandiko yake, Ukristo unaelezwa kama urithi wa kiroho uliojikita katika kutafuta ukweli na maadili safi, na unasaidia wafuasi wa dini tofauti kuelewana, ambapo upendo na kujitolea vinakuwa mhimili wa utume wa wateule wa Mungu.
Katika mahojiano na IQNA wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Nabii Isa (AS), Kaadi alisema:
“Ni lazima kusema kuwa Ukristo na Uislamu ni wenza katika njia ya imani na tauhidi. Kauli ‘Hakuna mungu ila Allah’ ilikuwepo katika Ukristo kabla ya Uislamu. Ukristo haujasahau kwamba mamajusi watatu kutoka nchi ya Iran walikuja Beit Lahm (Bethlehemu) kumpongeza Isa (AS) na walileta zawadi. Walipofika walisujujudu kwa heshima. Hakuna tofauti kati ya Ukristo na Uislamu, kwa sababu yeyote anayejisalimisha kwa Mungu bila shaka ni Mwislamu.”
Akaongeza:
“Katika hotuba na maandiko yangu kuhusu Ahlul-Bayt (SA), nasema kwamba sote ni Waislamu mbele ya Mungu na hakuna tofauti kati ya dini hizi mbili. Hapa ninaashiria mkutano wa Papa na Marja mkubwa wa Kishia Iraq, AyatUllah Sayyid Ali al-Sistani, kama ushahidi wa msingi kwamba Uislamu na Ukristo vina misingi ya kimungu na tauhidi ni moja.”
Kaadi alisisitiza kuwa Wakristo wengi, waandishi, washairi na wanahistoria zaidi ya 400, wameandika vitabu kuhusu Ahlul-Bayt na kutambua utakatifu wa Uislamu na Mtume Muhammad (SAW) aliyevunja masanamu kwa bendera ya tauhidi.
Alikiri:
“Nilimjua Isa kupitia aya za Qur’ani kabla ya Magharibi kumchora kwa simulizi za uongo. Baada ya kuisoma Qur’ani mara saba, nilitambua kuwa Mwenyezi Mungu amesema Isa ni Mtume wa Amani na Mtume wa Mungu duniani.”
Akanukuu Qur’ani (Surah Maryam: 33):
“Amani juu yangu siku nilipozaliwa, na siku nitakapokufa, na siku nitakapofufuliwa hai.”
Kwa mtazamo wake, mizizi ya Uislamu na Ukristo ni ile ile, na dini zote mbili zinatoka katika dini moja.
Kaadi aliendelea kusema:
“Isa (AS) tangu kuzaliwa alifundisha maadili ya kibinadamu na kubadilisha tabia mbovu za wanadamu, akawapa sura ya kimungu. Upendo wake kwa waja wa Mungu, kilio chake cha usawa na uadilifu, na mwongozo wake wa kijamii vyote vililenga kumuinua mwanadamu kufikia ukamilifu.”
Alisisitiza:
“Ni lazima tujifunze kupendana na kuthaminiana kwa kuiga maadili ya kibinadamu ambayo Ukristo ulifundisha, na Qur’ani Tukufu pia imeyataja. Ndiyo maana nasema nilijifunza Ukristo kutoka moyoni mwa Qur’ani.”
Kaadi alihitimisha kwa kusema:
“Utume wa Isa (AS) na Muhammad (SAW) ulikuwa wa kuhuisha na kukuza maumbile ya binadamu kwa misingi ya maadili ya kimungu. Qur’ani na Injili ni vitabu vya mbinguni vyenye funzo za maadili na elimu kwa maendeleo ya mwanadamu. Manabii wote wawili walijitolea maisha yao kuendeleza maadili na upendo wa kimungu. Hatupaswi kutofautisha kati ya Uislamu na Ukristo, kwa sababu lengo la zote ni upendo, rehema na kumtii Mungu Mmoja.”
3495847
Zenye maoni mengi zaidi