
Kwa mujibu wa Al‑Nahar, jumuiya hiyo imetoa taarifa ifuatayo kuhusu uvamizi wa Marekani dhidi ya Venezuela na vitisho vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran:
Inaonekana kwamba kiburi kilichomshika Rais wa Marekani, Donald Trump, kimemsukuma kuchukua hatua isiyo na heshima kwa sheria za kimataifa wala kwa matakwa ya mataifa. Adui huyu wa Kimarekani ameanzisha vita pana dhidi ya taifa huru la Venezuela. Kwa mtazamo wa Marekani, “kosa” la Venezuela ni kukataa kunyenyekea mbele ya matakwa ya Washington na kukataa kuruhusu utajiri wake kuporwa na makampuni ya Kimarekani.
Vikosi vya Marekani vimeanzisha mashambulizi makali dhidi ya Venezuela, vikilipua angalau malengo 11, yakiwemo majengo ya Bunge la Venezuela. Hali hii imemlazimu Rais Nicolás Maduro kutangaza hali ya hatari. Baadaye, vikosi vya Marekani vilimteka yeye na mke wake. Mataifa kadhaa yamelaani uvamizi huu unaoitumbukiza dunia katika “sheria ya msituni”. Kupitia kitendo hiki, Donald Trump anataka kupeleka ujumbe kwa wale wote wanaompinga kisiasa: kwamba mwisho wao utakuwa uvamizi na kutekwa kwa alama ya mamlaka ya kitaifa. Tukio hili linakuja sambamba na kumbukumbu ya kuuawa kwa shahidi Jenerali Qassem Soleimani na mwenzake Abu Mahdi al‑Muhandis — jambo ambalo si bahati mbaya, bali ni uthibitisho wa mwenendo huu wa Kimarekani.
Watu wa Venezuela na uongozi wao uliowekwa madarakani kwa uchaguzi watazima njama hii ya Marekani. Uvamizi huu utayalazimisha mataifa huru na yenye mamlaka kuungana dhidi ya dhulma hii ya Kimarekani na kuunda muungano wa kimkakati. Sisi, kama mkusanyiko wa wanazuoni wa Kiislamu, tunaona kwamba China, Urusi na Iran zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika harakati hii.
Wakati huohuo, Donald Trump ametangaza vitisho dhidi ya Iran. Hili linaashiria nia yake ya kuingilia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama alivyofanya Venezuela. Kwa hiyo, ni lazima tuwe macho na tayari kukabiliana na uingiliaji huo, ambao unaweza kuwa karibu iwapo mpango wa adui wa Kimarekani hautazuiwa na umakini wa watu wa Venezuela na Iran. Wale walioko mitaani Iran, wakidai kuwa na nia njema kwa kupinga baadhi ya sera za kiuchumi, wanapaswa kuwa waangalifu wasiruhusu harakati zao kutumiwa kuharibu nchi. Iran ni imara na ina uwezo wa kusimama kidete, na juhudi za Marekani dhidi yake zitafeli kama zilivyofeli Venezuela.
Jumuiya pia inatoa mwito kwa watu wa Iran na Venezuela kujitokeza kwa mamilioni mitaani kuunga mkono serikali zao halali dhidi ya uvamizi na kiburi cha Marekani. Yale anayofanya Donald Trump ni msumari mwingine katika jeneza la sera za Marekani, jambo litakalosababisha kuporomoka kwake pamoja na washirika wake wote, akiwemo utawala wa Kizayuni unaoendelea kupora ardhi — ambao wakati wake wa kusambaratika umeanza.
3495968