
Katika ujumbe wake kwa mkutano wa 59 wa kila mwaka wa Umoja wa Jumuiya za Wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya jana Jumamosi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Taifa la Iran kwa kutumia uwezo wake linaweza kusimama na kutoa wito wa thamani za Kiislamu kwa walimwengu kwa sauti kubwa kuliko wakati mwingine wowote."
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameangazia jukumu la vijana wa Iran katika kuzima mashambulizi makubwa ya jeshi la Marekani na "kitoto chake cha kuaibisha" katika eneo, akimaanisha utawala haramu wa Israel.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema mashambulio makubwa ya jeshi la Marekani na mwanaharamu wake katika eneo la Asia Magharibi yalishindwa kutokana na ubunifu, ushujaa na kujitolea kwa vijana wa Iran ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema katika ujumbe wake huo: "Wapendwa Vijana! Mwaka huu, nchi yenu, kutokana na imani, umoja na kujiamini, imepata hadhi na uzito mpya duniani. Uvamizi mkubwa wa jeshi la Marekani na kijitoto chake cha kuaibisha katika eneo hili ulishindwa kutokana na ubunifu, ushujaa na kujitolea kwa vijana wa Iran ya Kiislamu".
Ameongeza kuwa: Imethibitishwa kwamba taifa la Iran, kwa kutumia uwezo wake, chini ya kivuli cha imani na matendo mema, na katika kukabiliana na mabeberu waovu, linaweza kusimama kidete na kutoa wito wa thamani za Kiislamu kwa ulimwengu kwa sauti kubwa zaidi kuliko hapo awali.
Kadhalika Ayatullah Khamenei amesema kuwa, sababu kuu ya mkanganyiko wa mataifa ya kibeberu si mpango wa nyuklia wa Iran, bali ni msimamo wa nchi hii dhidi ya utaratibu usio wa kiadilifu na wa kiimla wa kimataifa na hatua yake ya kuanzisha mfumo wa kitaifa na kimataifa wenye msingi wa haki na uadilifu.
3495867