IQNA

Ansarullah ya Yemen

Shambulio dhidi ya Venezuela laonesha Marekani ni chhanzo cha uovu

20:28 - January 03, 2026
Habari ID: 3481758
IQNA – Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa tamko kali kulaani shambulio la kijeshi lililofanywa na Marekani dhidi ya Venezuela, ikilitaja kuwa kitendo cha jinai.

Tamko hilo limeeleza kuwa hujuma hiyo ni uvamizi wa wazi na wa kihalifu dhidi ya wananchi wa Venezuela, na ni ukiukaji wa dhahiri wa mamlaka ya taifa hilo pamoja na sheria na desturi za kimataifa.

Ansarullah imesema kuwa hatua za hivi karibuni za Marekani, ikiwemo shambulio la kijeshi, mzingiro wa anga, na kukamatwa na kuporwa kwa meli za mafuta za Venezuela, zinaonesha ukubwa wa ukatili wa Marekani na wigo wa jinai zake, na ni mfano mwingine wa sera za uharibifu za Washington dhidi ya mataifa na rasilimali zao.

Ansarullah imsisitiza kuwa mwenendo wa Washington dhidi ya Venezuela unathibitisha tena kwamba Marekani ndiyo chanzo cha uovu, shari, ugaidi na ufisadi duniani, na kwamba hutumia mantiki ya nguvu katika siasa zake za nje ili kutimiza malengo na mipango yake mibaya.

Harakati hiyo pia ilitangaza kuunga mkono Venezuela na rais wake, Nicolás Maduro, ambaye ametetea haki za wananchi wa Palestina pamoja na taifa lake. Aidha, ilisisitiza haki ya Venezuela kujilinda dhidi ya uvamizi wa Marekani na kulinda mamlaka yake, watu wake na rasilimali zake.

Tamko hilo liliitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kukomesha uvamizi huo wa Marekani na kuheshimu misingi na sheria za kimataifa zinazolinda mamlaka ya mataifa na maslahi ya wananchi.

Tamko la Trump

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba Marekani imefanya “shambulio kubwa la kijeshi” dhidi ya Venezuela na imemkamata Rais Maduro.

Trump alitoa tangazo hilo kupitia jukwaa lake la Truth Social mapema Jumamosi, muda mfupi baada ya milipuko mikubwa kuripotiwa katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas, ishara ya kuongezeka kwa hatua za kijeshi dhidi ya taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Trump alisema kuwa mke wa Maduro pia amekamatwa wakati wa operesheni hiyo na wote wawili “wamesafirishwa nje ya nchi.”

“Operesheni hii imefanywa kwa ushirikiano na 'vyombo vya sheria' vya Marekani,” Trump aliongeza.

Serikali ya Venezuela haijatoa tamko lolote kufuatia madai hayo mapya ya Trump. Hapo awali, iliripotiwa kuwa Maduro ametangaza hali ya dharura ya kitaifa kufuatia shambulio hilo.

Mamlaka za Venezuela ziliripoti kuwa mashambulizi yalifanyika Caracas siku ya Jumamosi, pamoja na katika majimbo ya Miranda, Aragua na La Guaira.

Maafisa hao walisema kuwa Washington imepanga mashambulizi hayo kwa lengo la kutwaa mafuta na madini ya Venezuela, wakiahidi kuwa juhudi hizo “hazitafanikiwa.”

Rais wa Marekani amekuwa akitoa vitisho mara kwa mara kuhusu mashambulio ya ardhini dhidi ya magenge ya dawa za kulevya katika eneo la Amerika ya Kusini, hususan Venezuela.

Katika mahojiano ya Alhamisi, Maduro alisema kuwa Venezuela iko tayari kuingia katika mazungumzo na Marekani kuhusu suala la biashara ya dawa za kulevya.

Katika mahojiano hayo, Maduro pia alidai kuwa Marekani inatafuta kuuangusha utawala wake na kutwaa akiba kubwa ya mafuta ya Venezuela kupitia vikwazo vya muda mrefu na kampeni ya shinikizo la kijeshi inayoratibiwa na Washington.

3495946

Habari zinazohusiana
captcha