Katika hatua hii, washiriki 16 wanashindana kwa makundi manne ya watu wanne, ambapo baadhi yao husoma Qur’ani kwa pamoja, na hatimaye mmoja huondolewa katika kila raundi.
Kipindi hiki pia kilihusisha washiriki wa Dawlat al-Tilawa kukutana na Waziri wa Awqaf wa Misri.
Ratiba ya Ijumaa ilirushwa saa tatu usiku kwa saa za Misri kupitia vituo vya Al-Hayat, CBC na Al-Nas, ambapo wasomaji wanne wenye sauti za kipekee walishindana, na kamati ya majaji ikakabiliwa na changamoto kubwa ya kuchagua bora zaidi.
Hatimaye, Muhammad Abu al-Alaa aliondolewa katika raundi hii. Kupitia ukurasa wake wa Facebook aliandika: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Leo ushiriki wangu katika Dawlat al-Tilawa umefikia tamati; lakini hii si mwisho wa kazi, bali ni ukamilifu wa tajriba ambayo nimeona jinsi Qur’ani inavyohifadhiwa inaposhughulikiwa na watu wake, na jinsi msomaji anavyoheshimiwa anapowekwa katika nafasi yake ya heshima.”
Qari huyo wa Misri alitoa shukrani kwa kamati ya majaji, Wizara ya Awqaf na Kampuni ya Al-Mutahida, akisema: “Niliondoka Dawlat al-Tilawa nikiwa na yakini kuwa usomaji wa Qur’ani wa Kimasri si shule ya sauti pekee. Bali ni urithi wa uelewa na adabu, usomaji unaojengwa juu ya elimu, ukipambwa kwa uaminifu na ikhlasi, na kuhitimishwa kwa unyenyekevu.”
Katika kipindi hicho, mtangazaji Ayyah Abdel Rahman alitambulisha Kituo cha Dar-ul-Qur’an cha Misri, kilichoko katika mji mkuu mpya wa kiutawala, akieleza kuwa ni jengo la kipekee la kidini na kitamaduni linaloonyesha ukubwa wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Aidha, kituo hicho kina makumbusho maalum ya maqari wa Kimasri, ambapo wageni hupata fursa ya kusikia sauti zao kana kwamba bado wako hai. Miongoni mwa kazi muhimu zaidi ni mswada mkubwa wa Kiosmani ulioandikwa kwa hati ya Kufi, wenye uzito wa kilo 80, unaochukuliwa kuwa hazina adimu ya sanaa ya Kiislamu na urembo wa kaligrafia ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa ripoti, Waziri wa Awqaf Osama Al-Azhari aliwapokea washiriki wa Dawlat al-Tilawa katika Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu nchini Misri.

Al-Azhari alisema: “Kuwachagua nyota wa Dawlat al-Tilawa ni jambo gumu, lakini hali ya mashindano inalazimisha. Wote ni watoto wangu na nina furaha kukutana nao, lazima tuwasaidie wote.”
Shindano hili linazalishwa kwa ushirikiano na Wizara ya Awqaf na Kampuni ya United Media Services, kwa lengo la kubaini vipaji na makari wa Qur’ani kutoka mikoa mbalimbali ya Misri.
Kipindi hurushwa kupitia vituo vya satelaiti vya Al-Hayat, CBC, Al-Nas, Misr Qur’an Karim na jukwaa la watch it, saa tatu usiku kila Ijumaa na Jumamosi.
Shindano linatoa jumla ya zawadi ya pauni milioni 3.5 za Kimasri. Washindi wa kwanza katika makundi ya usomaji na tajwid watapokea pauni milioni moja kila mmoja, na Qur’ani nzima itarekodiwa kwa sauti zao na kurushwa kupitia kituo cha Misr Qur’an Karim.
Aidha, watapewa heshima ya kuongoza Sala za Taraweeh katika Msikiti wa Hussein katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ujao.
Kamati ya majaji inajumuisha wanazuoni na viongozi mashuhuri wa Kiislamu: Hassan Abdel-Nabi, Taha Abdel-Wahab, Mostafa Hosny, na Taha Al-Nuamani. Wageni maalum ni pamoja na Osama al-Azhari, Nazir Mohamed Ayyad, Ali Gomaa, Ahmed Nuaina, Abdel-Fattah al-Tarouti, Jaber al-Baghdadi, mwanazuoni wa Uingereza Muhammad Ayoub Asif, na Qari wa Morocco Omar al-Qazabri.
4325263