IQNA

Mashia wafungua kituo cha kuhifadhi Qur'ani Saudia

10:29 - January 31, 2016
Habari ID: 3470103
Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia wamefungua kituo cha kuhifadhi Qur'ani mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Kituo cha Kuhifadhi Qur'ani na Sayansi za Qur'ani cha Al-Ahsa kimefunguliwa katika sherehe iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya maqarii na wasomi wa Kiislamu katika eneo hilo ambalo wakaazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Akihutubu katika kikao hicho, Khali Al Barrak, naibu gavana wa eneo hilo amesema kuanzishwa kwa vituo vya Qur'ani ni jambo ambalo litatoa huduma kwa jamii na kuimarisha itikadi za kidini. Ameongeza kuwa vituo kama hivyo vina nafasi katika kulea kizazi kinachoifahamu Qur'ani pasina kuwepo itikadi za misimamo mikali ya kidini.

Aidha ametoa wito kwa watu wenye uwezo, maafisa wa serikali na wanazuoni kuchangia kifedha na kimaanawi katika kuendeleza vituo vya Qur'ani.

Khalid al Barikan mkuu wa Baraza la Usimamizi wa kituo hicho amesema kuwa lengo muhimu zaidi la kituo hicho ni kufundisha Qur'ani kwa msingi wa kutafsiri na kutafakari kuhusu aya za Qur'ani. Aidha amesema wataalamu wa kituo hicho watasaidia katika kuboresha usomaji wa Qur'ani. Ameongeza kuwa kituo hicho ni wazi kwa watu wa matabaka yote ya umri.


captcha