Mmoja wa watoto hao ni Saji Ayash, aliyempoteza baba yake katika mashambulizi ya anga ya Israel katika miezi ya mwanzo ya vita. Akiwa kambini, alijiunga na mpango wa kuhifadhi Qur’ani katika kambi ya Al-Baraka kusini mwa Gaza, mpango unaowahudumia watoto yatima 500 wa kike na wa kiume.
Saji, ambaye tayari ni Hafidh wa Qur’ani, alieleza fahari yake: “Sisi ni watoto wa mashujaa waliouawa shahidi. Wazazi wetu walijitahidi sana ili tuhifadhi Qur’ani, ili tuwatie moyo na kuwavisha taji la heshima Siku ya Kiyama.”
Akaongeza: “Mimi kama binti wa shahidi, ninajivunia kuhifadhi na kusoma Qur’ani hapa kambini. Natumai kisomo changu kitakuwa chanzo cha fahari kwa baba yangu na thawabu kwake huko Peponi.”
Mshiriki mwingine, Saif Abu Bakr, ndiye pekee aliyenusurika katika familia yake. “Tulikuwa tunaishi kwa amani na furaha, lakini katika vita hivi baba, mama na dada zangu watatu waliuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel. Mimi nilinusurika nikiwa na majeraha na kuungua,” alisema. Licha ya maumivu, Saif alisisitiza azma yake: “Pamoja na dhulma, maumivu na njaa, nitaendelea kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kufuata mfano wa Mtume Muhammad (SAW) na kukamilisha.”
Muaz Abu Ajwah, yatima mwingine aliyeshiriki hafla ya kumaliza kuhifadhi Qur’ani, alitokwa na machozi alipomkumbuka baba yake. “Ninahifadhi Qur’ani na kushiriki hafla hii ili niwasilishe thawabu kwa baba yangu huko Peponi,” alisema. “Licha ya maumivu na kupoteza, nitaendelea na safari yangu ya Qur’ani ili kumfurahisha baba yangu huko Peponi na kumfikishia thawabu ya kuhifadhi na kisomo changu.”
Jitihada zao zinakuja wakati Wizara ya Wakfu na Mambo ya Kidini ya Gaza ikiripoti kuwa zaidi ya asilimia 90 ya misikiti katika Ukanda huo imeharibiwa, na hivyo kuwalazimu Wapalestina kubadilisha mahema ya wakimbizi kuwa sehemu za ibada na masomo ya Qur’ani.
Mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 65,000 tangu kuanza kwa vita mwezi Oktoba 2023. Mashambulizi hayo yasiyokoma yamewafanya karibu watu wote milioni 2.2 wa Gaza kuwa wakimbizi wa ndani, huku mzingiro mkali wa Israeli ukisababisha njaa kali katika eneo hili.
4305605