
Rais Rouhani amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa
pamoja na mgeni wake Rais John Dramani Mahama wa Ghana aliyeko hapa
nchini kwa ziara rasmi. Rais Rouhani amesema kuwa, katika mazungumzo
yake na Rais wa Ghana wamebadilishana mawazo kuhusiana na masuala ya
kieneo na kimataifa na kwamba, Tehran na Accra zimetiliana saini hati
kadhaa za ushirikiano katika masuala mbalimbali katika nyuga za kilimo,
mafuta, nishati, kakao, nishati jadidika na kadhalika. Rais wa Iran
ameashiria harakati za jihadi ya ujenzi za Iran huko Ghana na kusema
kuwa, kuanzishwa shule na vituo vya afya vya Iran katika nchi hiyo ya
magharibi mwa Afrika ni hatua muhimu. Rais wa Iran amesema kuwa, suala
la usalama wa kaskazini mwa Afrika na harakati za makundi ya kigaidi ni
mambo mengine aliyojadiliana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana na
kwamba, pande mbili zimesisitiza juu ya ulazima wa kupambana na ugaidi.
Aidha suala la Palestina na dhulma wanayotendewa wananchi hao madhlumu
ni suala lililotawala katika mazungumzo ya leo ya Marais wa Iran na
Ghana. Kwa upande wake Rais Dramani Mahama wa Ghana amepongeza mafanikio
ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na kubainisha kwamba, taifa hili
daima limekuwa muungaji mkono wa wananchi madhulumu wa Afrika katika
kupambana na ubaguzi.
3475559