IQNA

Raundi ya Mwisho ya Mashindano ya Qur'ani ya Sheikha Hind bint Maktoum huko Dubai

23:28 - October 15, 2025
Habari ID: 3481372
IQNA – Hatua ya mwisho ya Mashindano ya 26 ya Qur'ani Tukufu ya Sheikha Hind bint Maktoum imeanza rasmi Dubai, ikiwakutanisha wanaume na wanawake wanaohifadhi Qur’ani kutoka kote katika Muungano wa Falme za Kiarabu.

Mashindano haya yanaandaliwa na Tuzo ya Kimataifa ya Qur;ani ya Dubai chini ya Idara ya Masuala ya Kiislamu na Misaada ya Kijamii, na yataendelea hadi tarehe 23 Oktoba katika makao makuu ya tuzo hiyo.

Lengo kuu la tukio hili ni kuwahamasisha raia wa Emirati na wakazi wa taifa hilo, wanaume kwa wanawake, kuboresha usomaji na uhifadhi wa Qur’ani Tukufu kwa kufuata kanuni za Tajwidi. Washiriki wanapimwa kwa ubora wa kuhifadhi, usahihi wa aya, na ufasaha wa sauti katika mfumo wa mashindano ulio wazi na wa haki.

Kwa mujibu wa waandaaji, zaidi ya watu 1,660 walijiandikisha kwa awamu ya awali mwaka huu, wakiwemo wanaume 868 na wanawake 798. Jumla ya washiriki 1,514 walitimiza masharti ya kushiriki, wakihusisha asilimia 52 wanaume na asilimia 48 wanawake.

Washiriki walitoka katika mataifa 55, ambapo Wamirati waliongoza kwa idadi kubwa ya washiriki 1,028. Wengine walitoka Misri, India, Pakistan, Syria, na nchi nyingine kadhaa.

Ibrahim Jassim Al Mansoori, Mkurugenzi wa Muda wa Tuzo ya Kimataifa ya Qur'ani ya Dubai, alisema toleo la mwaka 2025 limevutia “ushiriki wa kipekee,” likionyesha umaarufu wa tukio hilo miongoni mwa vizazi mbalimbali.

Al Mansoori pia alisisitiza kuanzishwa kwa teknolojia mpya ni jambo linaloongeza uwazi na usawa katika mchakato wa tathmini.

3495025

captcha