IQNA

Utawala wa Aal Khalifa washindwa kuzuia Sala ya Ijumaa Bahrain

16:14 - February 27, 2016
Habari ID: 3470164
Hatua za askari polisi wa utawala wa Aal Khalifa za kutaka kuwazuia wananchi wa Bahrain wasishiriki kwenye Sala ya Ijumaa zimegonga mwamba.

Askari hao walishindwa kuwazuia waumini kushiriki kwenye Sala hiyo ambayo ilisaliwa kwa wito uliotolewa na maulamaa wa nchi hiyo.

Katika kuendeleza sera za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa, askari polisi wa utawala huo jana asubuhi walizifunga njia zote zinazoelekea eneo la Addaraz mahala alikozaliwa Sheikh Ali Salman, kiongozi mwandamizi wa upinzania na  Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Al-Wifaq ili kuzuia kusaliwa Sala ya Ijumaa katika eneo hilo.

Hata hivyo bila kujali hatua za askari hao, wananchi wa Bahrain walisali sala hiyo katika barabara za kandokando ya msikiti wa Imam Sadiq (AS) katika eneo la Addaraz huko magharibi mwa mji mkuu Manama, sala ambayo iliyosalishwa na Allamah Sheikh Muhammad Sanqur.

Tangu mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa malalamiko ya wananchi dhidi ya siasa za utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa. Mauaji, ukandamizaji na utiaji nguvuni watu yamekuwa ndio maelekezo makuu yanayotekelezwa muda wote na vikosi vya polisi ya utawala huo wa kifamilia.

Matukio yanayojiri nchini Bahrain yanaonyesha kuwa utawala wa Aal Khalifa unazidisha hatua za ukandamizaji dhidi ya wananchi kiasi kwamba kuwatia nguvuni na kuwafungulia kesi wanaharakati wa kisiasa kunazidi kuchukua sura pana zaidi inayozidi kutia wasiwasi siku baada ya siku.

Ripoti kutoka nchini humo zinaeleza kuwa kumeanza duru mpya ya utoaji hukumu za kidhalimu dhidi ya wanaharakati wa kisiasa, sambamba na utawala wa Aal Khalifa kuendeleza siasa zake za kidikteta kuhusiana na kuwaweka mahabusu wanaharakati wa kisiasa na viongozi wa mapambano ya wananchi; hali ambayo imeibua wimbi kubwa la malalamiko ya wafungwa wa kisiasa nchini humo.

Mwenendo wa utawala wa Aal Khalifa unaonyesha kuwa sio tu utawala huo wa kiimla unawanyima uhuru wa kisiasa wananchi wa Bahrain bali pia unakandamiza hata haki zao nyengine za msingi zikiwemo za uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu. Siasa za utawala wa Aal Khalifa zimesimama juu ya msingi wa kuzidi kuvunjia heshima itikadi za wananchi wa Bahrain hususan za Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao ndio wanaounda sehemu kubwa ya jamii ya nchi hiyo.


3478496

 

captcha