Walioshuhudia tukio hilo wanasema magaidi waliotekeleza unyama wa kuwaua waumini watatu kwa mapanga walikuwa na bendera za kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.
Mmoja wa manusura alisema, "Walikuwa watu 15 waliofunika sura zao zisionekane wakati wakivamia msikiti." Msikiti uliohujumiwa unajulikana kama‘Masjid Rahma’ mkoani Mwanza,eneo la Ibanda Relini, kata ya Mkolani wilayani Nyamagana.Aidha amesema washambuliaji hao walizima taa za msikiti kabla ya kuwaamuru watoto waondoke kupitia mlango ambao hutumiwa na wanawake na punde baada ya hapo wakaanza kuwakata kwa mapanga wanaume waliokuwa ndani ya msikiti. Ameongeza kuwa magaidi hao walikasirishwa na waumini wa msikiti huo kuswali ilihali kulikuwa na watu ambao walikuwa wamekamatwa na polisi. Baadhi ya walioshuhudia wanasema genge hilo liliongozwa na mwanamke aliyeamuru mauaji yatekelezwe. Baadhi ya duru zinasema magaidi hao walikuwa na bunduki za rashasha.
Mkuu wa Polisi eneo la Mwanza Ahmad Msangi amethibitisha kuwa watu watatu waliuawa katika msikiti huo katika hujuma iliyotekelezwa kwa mapanga. Ameongeza kuwa, polisi wanachunguza chanzo cha shambulizi hilo. Msangi amesema mashambulio hayo yanashabihiana na yale yanayotekelezwa na kundi la kigaidi la Al Shabaab huko Somalia na nchi jirani ya Kenya.
Rais John Magufuli wa Tanzania ametuma salamu za pole kufuatia mauaji hayo msikitini na ameviagiza vyombo vya dola kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika katika mauaji hayo. Polisi tayari wamesema wanawashikilia washukiwa kadhaa kufuatia tukio hilo.
AidhaShekh Hussein Ibrahim, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Nyamagana mbali na kulaani kitendo hicho, amesema vitendo vya namna hiyo havikubaliki katika Dini ya Kiislamu na kwamba, Waislamu wote wanapaswa kulaani matukio ya namna hiyo.