IQNA

Ustadh Ahmed Ahmed Nuaina

Waislamu watekeleze mafundisho ya Qur’ani katika sekta zote za maisha

9:32 - August 17, 2016
Habari ID: 3470527
Qarii mashuhuri wa Qur’ani Tukufu kutoka Misri amesema mafundisho ya Qur’ani yanapaswa kutekelezwa katika sekta zote za maisha.

Akizungumza na IQNA, Ustadh Ahmed Ahmed Nuaina amesema Umma wa Kiislamu unapaswa kuendesha mambo yake yote kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu.

Akijibu swali kuhusu ni vipi Waislamu wakabiliana na hujuma ya kiutamaduni na kiaidiolojia ya madola ya Magharibi dhidi ya Umma wa Kiislamu, Ustadh Nuaina amesema Waislamu wanapaswa kutumia akili na mantiki ya Kiislamu kukabiliana na hali hiyo.

Ameashiria aya ya 125 ya Sura Nahl katika Qur’ani Tukufu isemayo: "Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.”

Ustadh Nuaina amesema ayah hii inaonyesha njia bora zaidi ya kukabiliana na madola ya Magharibi.

Kwingineko qarii huyo mashuhuru wa Misri ameashiria aya za Qur’ani zinazosisitiza kuhusu umuhimu wa kulinda familia na kuwaheshimu wazazi.

Ustadh Nuaina ameangazia aya ya 23 ya Sura al Isra katika Qur’ani Tukufu isemayo: "Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.”

Ustadh Nuaina alizaliwa mwaka 1954 katika mji wa Mutubas nchini Misri na alianza kujifunza Qur’ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 4 na kuhifadhi Kitabu hicho Kitukufu akiwa na umri wa miaka minane.

Alijifunza mbinu ya qiraa ya Ustadh Mustafa Ismail huku akiendeleza masomo yake katika taalumu ya daktari wa watoto.

Noaina anatambuliwa kama mmoja kati ya wasomaji bora zaidi wa Qur’ani Misri na ulimwengu mzima katika zama hizi.

3460711

captcha