Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Ashraf, mwenye umri wa miaka 23, anaishi katika kijiji kimoja kilichopo katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini na amepata umashuhuri kiasi cha Wizara ya Awqaf ya Misri kumtaja kuwa miongoni mwa quraa 50 bora wa Qur'ani nchini humo.
Katika mahojiano na tovuti ya al-Misriyun, Ustadh Ashraf amebaiisha mafanikio yake katika usomaji Qur'ani. Anasema alilelewa katika familia yenye kuzingatia misingi ya Qur'ani. Baba yake alikuwa mwalimu wa Qur'ani katika kituo cha Chuo Kikuu cha Al Azhar mbali na kuwa qarii katika msikiti wa al Kawakibi. Aidha anasema babu yake aliwahi kutajwa kuwa Sheikh al Quraa, yaani qari bora zaidi, katika mkoa wa Giza. Ustadh Ashraf ambaye wajomba zake wote pia walikuwa wamehifadhi Qur'ani alizaliwa mwaka 1994 katika kijiji cha Nahiya mkoani Giza. Anasema alianza kuhifadhi Qur'ani akiwa na umri wa miaka mine. Baadaye alifanikiwa kuhifadhi Qur'ani kikamilifu na akaanza kupata umashuhuri kama qarii huko Giza na maeneo mengine ya Misri.
Aidha anasema anavutiwa na anaiga mbinu ya qiraa ya marehemu Ustadh Shahat Mohammad Anwar. Ashraf anasisitiza kuhusu mapenzi yake kwa Qur'ani Tukufu na kuongeza kuwa amepita njia ngumu kabla ya kufika alipo hivi sasa kama qarii na hafidh wa Qur'ani Tukufu. Anasema hivi sasa ana uhusiano mzuri wa kimaanawi na mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
3462097