IQNA

Wafungwa 21,000 wahifadhi Qur'ani nchini Iran

14:48 - January 01, 2018
Habari ID: 3471338
TEHRAN (IQNA)-Wafungwa 21,000 wanaohudumu vifungo nchini Iran wamehifadhi Qur'ani Tukufu katika viwango mbali mbali.

Hayo yamedokezwa na Hujjatul Islam Ridha Rostami, mkurugenzi wa Kitengo cha Utamaduni na Elimu katika Idara ya Magereza nchini Iran. Ameongeza kuwa, wafungwa wengine 90,000 wanaendelea na darsa za Qur'ani zilizoandaliwa na kitengo hicho.

Amebaini kuwa kutokana na taathira chanya, wanaojifunza Qur'ani na kuihifadhi wanapoachiliwa huru ni nadra kurejea tena gerezani na kiwango hicho sasa ni chini ya asilimia 2.

Hujjatul Rostami pia ameashiria kuhusu harakati za kidini katika magereza kote Iran na kuongeza kuwa wafungwa wenyewe wameonyesha raghba na shauku kubwa ya kushiriki katika vikao na hafla za kidini.

Amesema mwaka jana kulikuwa na tamasha la Qur'ani liloloandaliwa na idara ya magereza katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran ambapo washiriki waliweza kupata mafunzo mengi. Halikadhalika amesema Idara ya Magereza Iran imeanzisha vituo 294 vya mafunzo ya Qur'ani vijulikanavyo kama Darul Qur'an katika magereza kote nchini huku hakisisitiza umuhimu wa kuwepo vituo kama hivyo ili kurekebisha kimsingi tabia za wafungwa.

3464823

captcha