IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na rais wa Uturuki
22:29 - September 07, 2018
News ID: 3471662
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hitajio muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu hii leo ni ukuruba zaidi na mshikamano wa nchi za Kiislamu.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo alasiri hapa mjini Tehran alipokutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na ujumbe aliokuwa ameandamana nao. Kiongozi Muadhamu amesema nchi za Kiislamu bila ya shaka zitaandaa mazingira ya kutatuliwa matatizo ya eneo. Amesema ni kwa sababu hiyo ndio maana madola ya kiistikbari yakiongozwa na Marekani yana wasiwasi kutokana na ushirikiano na ukuruba wa nchi za Kiislamu sambamba na kupatikana umma wenye nguvu wa Kiislamu.

Ayatullah Khamenei amesema uhasama na hila ya Marekani kwa nchi za Kiislamu zenye nguvu ni ishara ya wasiwasi huo. Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki ni nchi mbili zenye heshima na nguvu katika eneo na zina motisha kwa ajili ya ulimwengu wa Kiislamu na kwa msingi huo zinapaswa kushirikiana katika nyuga za kisiasa na kiuchumi zaidi ya huko nyuma.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki tokea uingie madarakani mrengo wa Kiislamu nchini humo na kusema kuna haja ya kuimarisha nukta za pamoja baina ya nchi mbili.

Ayatullah Khamenei aidha amepongeza msimamo wa Rais Erdogan kuhusu suala ya Myanmar na ameashiria kadhia ya Palestina na kusema: "Kadhia ya Palestina ni muhimu na haipaswi kughafilika na suala hilo hata kwa lahadha moja."

Katika mazungumzo hayo, Rais wa Uturuki amesema hali ya hivi sasa katika eneo hili ni ya mgogoro na ameelezea matumaini yake kuwa, kwa ushirikiano wa nchi za Kiislamu mgogoro huo utaweza kutatuliwa.

Rais Erdogan aidha amesema, mgawanyiko na kukosekana mshikamano baina ya nchi za Kiislamu ni moja ya sababu za kujitokeza hali iliyopo hivi sasa. Aidha amesema kutokana na sera za nchi za Magharibi dhidi ya nchi za Kiislamu zenye misimamo huru, hali imezidi kuwa nyeti na kwa hivyo kuna haja ya kuimarishwa mshikamano na udugu baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki.

3744716

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: