IQNA

Qarii mashuhuri wa Tanzania Ustadh Rajayi Ayoub
21:22 - April 13, 2019
News ID: 3471915
TEHRAN (IQNA)- Qarii mashuhuri wa Qur'ani Tukufu kutoka nchini Tanzania Ustadh Rajayi Ayoub amesema Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran ni fursa muhimu ya kuleta umoja miongoni mwa Waislamu duniani.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa IQNA, Ustadh Ayoub ambaye ni mgeni wa heshima katika Mashindano ya 36 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran ameongeza kuwa,  Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yameweza kuleta umoja na kuwaunganisha Waislamu wa madehehbu mbali mbali duniani. Ameendelea kusema kuwa, "Mashindano ya Qu'rani ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran ni njia muhimu sana ya kuwaunganisha Waislamu. Kwanza wanaunganishwa kwa njia ya kheri, yaani kupitia usomaji Qur'ani Tukufu."

Aidha qarii huyo mashuhuri wa Qur'ani Tukufu kutoka Tanzania amebanisha kuridhishwa kwake na kiwango cha mashindano ya mwaka hii na kuongeza kuwa, "Mashindano ya kimataifa ya Qur'ani  ya Iran mwaka huu yameboreka zaidi hasa kutokana na hatua ya Iran kuongezwa vitengo maalumu vya washiriki wanawake, wanafunzi wa shule, walemava wa macho na wanafunzi wa vyuo vya kidini."

Halikadhalika Ustadh Rajayi Ayoub ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa  mwaliko wa kuwa mgeni wa heshima na msomaji maalumu katika Mashindano ya 36 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu. Amesema mwaliko huo pia ni heshima kubwa kwa taifa la Tanzania. Siku ya Alhamisi, baada ya kumalizika siku ya pili ya Mashindano ya 36 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran, Ustadh Ayoub alipata fursa ya kusoma aya za Qur'ani mbele ya hadhirina katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA kabla ya adhana ya Sala ya Magharibi.

Mwaka huu washiriki 184 wa mashindano ya Qur'ani kutoka nchi 84 walifanikiwa kufika katika nusu fainali ya mashindano ya mwaka huu.

Nusu fainali ya mashindano hayo ilifanyika Jumanne Aprili 9 na Jumatano Aprili 10 asubuhi kabla ya ufunguzi rasmi wa fainali alasiri ya Jumatano ambapo inatazamiwa kuwa mashindano yatamalizika Aprili 14.

Hapa chini ni video ya Qiraa ya Ustadh Rajayi Ayoub

Name:
Email:
* Comment: