IQNA

14:38 - June 19, 2019
News ID: 3472007
TEHRAN (IQNA) – Marekani inaendelea kuficha jinai za kivita za utawala wa Saudia Arabia na waitifaki wake ambao wanaendelea na uvamizi wao dhidi ya taifa la Yemen.

Katika hatua ya hivi karibuni kabisa ya kuficha jinai hizo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ameliondoa jina la Saudi Arabia katika orodha ya Washington ya nchi zinazowasajili watoto jeshini.

Pompeo amechukua hatua hiyo, licha ya ripoti ya wataalamu wa Ofisi ya Kupambana na Magendo ya Binadamu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kusisitiza kuwa, Riyadh inasawasajili watoto ndani ya jeshi lake hususan kutoka Sudan, na kisha kuwatumia katika vita vyake dhidi ya raia wa Yemen.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani waliopinga ripoti ya wataalamu wa Ofisi ya Kupambana na Magendo ya Binadamu ya wizara hiyo wamedai kuwa, askari mamluki kutoka Sudan wako chini ya amri na maagizo ya Jeshi la Sudan na wala sio chini ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na Imarati.

Disemba 28 mwaka jana, gazeti la The New York Times linalochapishwa nchini Marekani liliripoti kuwa, kwa sababu ya pesa, askari watoto kutoka eneo la Darfur nchini Sudan wanapigana mstari wa mbele kwa niaba ya Saudi Arabia na waitifaki wake katika vita vya umwagaji mkubwa wa damu vilivyoanzishwa na Riyadh dhidi ya Yemen.

Wanamgambo wawili wa Sudan waliorudi makwao kutoka vitani nchini Yemen waliliambia gazeti la New York Times kuwa, zaidi ya asilimia 40 ya askari waliokuwa kwenye kikosi chao walikuwa watoto wadogo.

Ripoti ya gazeti hilo aidha ilifichua kuwa, baadhi ya familia za Wasudan hutoa hongo kwa maafisa wa makundi ya wanamgambo ili vijana wao wapate fursa ya kwenda vitani nchini Yemen.

Vita vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen vilianza tarehe 26 Machi mwaka 2015, na sasa viko katika mwaka wake wa tano.

Wakati Saudia ilipoanzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo masikini zaidi ya Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi, ilikuwa imetathmini kuwa vita hivyo havitaendelea kwa zaidi ya wiki tatu. Lengo kuu la Saudia katika kuanzisha vita hivyo lilikuwa ni kuiondoa harakati ya Ansarullah madarakani na kuifanya irejee katika hali ya kutengwa kama ilivyokuwa kabla ya mwezi Septemba mwaka 2014. Hivi sasa miaka minne baada ya vita hivyo haramu, si tu kuwa Ansarullah haijarejea katika hali ya kabla ya Septemba 2014, bali hivi sasa Ansarullah ni mhimili mkuu wa nguvu na utawala nchini Yemen na hakuna mazungumzo yanayoweza kufanyika Yemen pasina kuishirikisha harakati hiyo.

Mbali na hayo, ukoo wa Aal Saud unaotawala Saudia, baada ya kuanzisha vita dhidi ya Yemen ulitangaza kuwa lengo la vita hivyo ni kurejesha kile ulichodai kuwa ni "uhalali" na hapo kusudio lilikuwa ni kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyejuzulu kama rais wa Yemen na kutoroka nchi, Abdu Rabbuh Mansour Hadi.

Hivi sasa baada ya kumalizika mwaka wa nne wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen, Mansour Hadi bado yuko Riyadh na si tu kuwa hajaweza kurejea Sanaa bali kwa mtazamo wa Wayemen waliowengi, amefanya uhaini mkubwa kwa kuunga mkono vita vya Saudia ambavyo vimesababisha umwagaji damu ya wananchi wasio na hatia.

Saudi Arabia na waitifaki wake katika vita vya Yemen wametenda jinai kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC. Jinai hizo ni pamoja na jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu, jinai dhidi ya amani na jinai ya uvamizi. Kuna nyaraka na ushahidi wa wazi kuhusu jinai hizo za Saudia na waitifaki wake dhidi ya watu wa Yemen.

Yusuf Al Hadhri, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Yemen katika taarifa kuhusu vita vya Saudia dhidi ya Yemen amesema, katika kipindi cha miaka minne ya vita hivyo watu  12,000 wameuawa moja kwa moja vitani huku wengine 26,000 wakiwa wamejeruhiwa. Aidha amesema katika kipindi hicho, wagonjwa 32,000 Wayemen wameaga dunia kutokana na kuwa hawawezi kuenda nje ya nchi kupata matibabu kufuatia mzingiro uliowekwa na muungano huo vamizi wa Saudia. Kwa maneno mengine ni kuwa watu 44,000 wamefariki dunia nchini Yemen kutokana na vita kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Miongoni mwa waliofariki kuna wanawake na watoto 6,361.

346878

Name:
Email:
* Comment: