IQNA

9:12 - August 07, 2019
News ID: 3472073
TEHRAN (IQNA) - Wananchi wa Nigeria wamemiminika mabarabarani na kusherehekea kwa nderemo na vifijo kutangazwa hukumu ya kuachiwa huru kwa dhamana kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky ili asafiri kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Jana Jumatatu mahakama ya Nigeria katika jimbo la Kaduna ilitoa ruhusa kwa Sheikh Zakzaky na mkewe ya kusafiri kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kuhusiana na suala hilo Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeeleza kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba, kiongozi wao huyo sasa ameruhusiwa yeye pamoja na mkewe kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa harakati hiyo, mara baada ya kuachiliwa huru, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wanatarajiwa kusafiri kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu.

Wanigeria wamiminika mabarabarani kusherehekea kuachiwa huru kwa dhamana Sheikh Zakzaky

Tovuti ya gazeti la Vanguard linalochapishwa nchini Nigeria nayo pia imetangaza kuwa, safari ya Sheikh Zakzaky kuelekea India itafanyika kwa masharti maalumu, likiwemo la kuandamana maafisa wa usalama wa Nigeria na kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo katika safari yake hiyo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe walitiwa nguvuni na askari wa jeshi la Nigeria Desemba 13, 2015 katika shambulio na uvamizi uliofanywa na askari hao dhidi ya Hussainiya ya mji wa Zaria nchini humo.

Siku waliyomtia nguvuni Sheikh Zakzaky, askari wa jeshi la Nigeria waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wamejumuika kwenye Hussainiya hiyo na mbele ya nyumba ya kiongozi huyo wa kidini na kuwaua shahidi mamia miongoni mwao wakiwemo watoto wake watatu wa kiume.

Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016 na kuliwajibisha jeshi la nchi hiyo kulipa fidia ya dola laki moja na 50 elfu kwa familia ya Sheikh Zakzaky. Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vya Nigeria vilikataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama na kuendelea kumweka korokoroni mwanchuoni huyo kinyume cha sheria.

http://parstoday.com

Name:
Email:
* Comment: