IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
22:09 - October 19, 2019
News ID: 3472180
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa iwapo vijana watasimama kidete katika njia iliyonyooka na ya haki, basi wataweza kuleta mabadiliko katika taifa la Iran na dunia nzima kwa ujumla.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo mapema leo Jumamosi katika marasimu ya maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS akiwa pamoja na kundi la wanafunzi wa vyuo vikuu katika Hussayniyah ya Imam Khomeini MA hapa jijini Tehran.

Kiongozi Muadhamu ametoa hotuba fupi mbele ya wanachuo hao ambapo amesisitiza kwamba, "Daima namuomba Allah anisimamishe kidete mimi na nyinyi katika njia iliyo sawa, kwa kuwa kusimama imara katika njia hiyo kutaleta marekebisho katika nchi hii na dunia; na jamii yote ya mwanadamu itaweza kustafidi na natija ya kusimama kidete huko."

Kadhalika Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza tabaka la vijana wa Iran kwa kushiriki kwa moyo wa dhati kwenye maombolezo hayo ya Arubaini ya Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW.

Kwingineko, matembezi ya "Waliosalia Nyuma" katika Arubaini ya Imam Hussein AS yamefanyika katika mwendo wa kilomita 17 kuanzia kwenye medani ya Imam Hussein AS hapa mjini Tehran kuelekea haram ya mtukufu Abdul-Adhim AS iliyoko mjini Rey kusini mwa Tehran kwa kuhudhuriwa na wapenzi na maashiki wa Imam Hussein AS

Naibu wa Meya wa jiji la Tehran, Mojtaba Yazdani amesema, askari wapatao 450 na magari yapatayo 205 yamesindikiza matembezi hayo kwa ajili ya kutoa huduma kwa waumini.

Sambamba na kukaribia kufanyika matembezi makubwa ya "Waliosalia Nyuma" katika Arubaini, asubuhi ya jana, ilifanyika shughuli ya kuinadhifisha na kuinukisha kwa manukato haram toharifu ya mtukufu Abdul-Adhim al-Hassani AS iliyopo mjini Rey kwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wafuasi na maashiki wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW.

Leo Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Tano, Safar, mwaka 1440 Hijria inayosadifiana na Oktoba 19, mwaka 2019 Miladia ni Siku ya Arubaini ya Imam Hussein (as), Imam wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na wafuasi wake waaminifu na watiifu waliouawa shahidi katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria.

3850890/

Name:
Email:
* Comment: