IQNA

Rais Rouhani wa Iran
12:54 - January 11, 2020
News ID: 3472361
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kosa la kibinadamu lililotokana na vitisho vya Marekani vya kushambulia maeneo nyeti nchini Iran ndiyo sababu ya kuanguka ndege ya abiria ya Ukraine karibu na Tehran.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo katika taarifa yake ya leo Jumamosi na huku akigusia tamko lililotolewa na Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Iran kuhusu ajali hiyo, ameelezea kusikitishwa sana na ajali hiyo na kutoa mkono wa pole kwa mataifa, tawala na familia za wahanga wa ajali hiyo akisema: Baada ya utawala vamizi wa Marekani kuzusha hali ya vitisho dhidi ya taifa la Iran, majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliwekwa kwenye hali ya tahadhari kubwa ya kujilinda na shambulizi lolote la Marekani na kwa masikitiko ni kwamba katika hali hiyo ya wasiwasi mkubwa, kulitokea kosa la kiibinadamu na kusababisha maafa makubwa ya kupoteza maisha makumi ya watu wasio na hatia.

Rais Rouhani ameongeza kuwa, uchunguzi unaendelea kuhusu sababu zote zilizopelekea kutokea maafa hayo na wahusika wa kosa hilo la kusikitisha watafuatiliwa na sheria na matokeo ya uchunguzi huyo litaelezwa taifa la Iran na familia za wahanga wa ajali hiyo.

Kwa upande wake, Dk Mohamad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema leo katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, kosa la kibinadamu lililotokea wakati kama huo wa vitisho vya Marekani ndiyo sababu kuu ya ajali hiyo.

Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Iran leo Jumamosi imetoa taarifa rasmi na huku ikiashiria vitisho vya rais wa Marekani na majenerali wa kijeshi wa nchi hiyo vya kushambulia maeneo kadhaa muhimu ndani ya ardhi ya Iran sambamba na kuongezeka ndege za kijeshi za magaidi wa Marekani zilizokuwa zinaruka wakati huo karibu na Iran, katika mazingira kama hayo, kulitokea kosa la kibinadamu lililopelekea kutunguliwa ndege hiyo baada ya kukaribia sana katika kituo kimoja nyeti cha kijeshi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.

Jumatano asubuhi, ndege moja ya abiria ya shirika la ndege la Ukraine aina ya Boing 737 ilianguka karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran, ambapo abiria wote 167 pamoja na wahudumu 9 waliokuwemo ndani yake walifariki dunia.

Tukio hilo lilijiri masaa machache baada Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC,  katika kujibu jinai na ugaidi wa wanajeshi vamizi wa Marekani ambao walimuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, lilivurumisha makombora ambayo yamelenga kituo cha anga cha jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani cha Ain al-Assad nchini Iraq.

3870581

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: