IQNA

Mamilioni ya Wairaqi waandamana, wataka askari vamizi wa Marekani waondoke

21:22 - January 24, 2020
Habari ID: 3472402
TEHRAN (IQNA) - Mamilioni ya wananchi wa Iraq leo Ijumaa wameandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad wakitaka kuondoka nchini humo wanajeshi wa Marekani kufuatia shambulio kubwa la kigaidi lililofanywa na Marekani hivi karibuni nchini humo.

Kwa kufanya maandamano hayo ya leo, wananchi wa Iraq wamedhihirisha nguvu ya Uislamu na taifa kubwa la Iraq dhidi ya nchi vamizi Marekani na waitifaki wake. Sadiq al Hashemi Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Iraq amesema kuwa Wairaqi zaidi ya milioni 2 na nusu wameshiriki maandamano hayo ya leo. 

Makundi ya muqawama wa Kiislamu, shakhsiya wa kidini na viongozi wa kisiasa na kitaifa wa Iraq wameyataja maandamano hayo dhidi ya uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini humo kuwa ni "Siku ya Mamlaka ya Kitaifa", huku wengine wakisema kuwa yanafanana na mapinduzi ya mwaka 1920 na kuondoka kwa madhila mkoloni Muingereza nchini Iraq.

Kuanzia saa za awali za leo, wimbi kubwa la wanaume, wanawake na watoto wa kaumu zote za Iraq walimiminika kwa wingi katika kitongoji cha Jadriyah karibu na Chuo Kikuu cha Baghdad. Wananchi wa Iraq walikuwa wamebeba mabango na kupiga nara wakitaka kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini humo. Aidha walipiga nara za Mauti kwa Marekani na Mauti kwa Israel na kudhihirisha hasira na chuki yao kwa wanajeshi wavamizi. Mtandao wa habari wa al Ahd wa Iraq umeripoti kuwa matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iraq kutoka miji mbalimbali ya nchi hiyo wameshiriki katika maandamano ya leo huko Baghdad.  

Sambamba na maandamano hayo ya leo, Muqtada Sadr Mkuu wa Mrengo wa Sadr nchini Iraq ametoa taarifa akitaka kufutwa makubaliano yote ya kiusalama yaliyofikiwa kati ya Iraq na Marekani na kusisitiza kuwa, serikali inapasa kufunga kambi zote za kijeshi za Marekani zilizopo nchini humo. Amesema wataamiliana na Marekani kama nchi vamizi na adui iwapo Wamarekani hawatakuwa tayari kuondoka Iraq.   

Muqtada Sadr ameongeza kuwa, Baghdad inapasa kufunga anga ya nchi hiyo mbele ya oparesheni za kijeshi za Marekani na kwamba kuondoka Marekani nchini humo hakuwezi kutimia isipokuwa kwa kufungwa kambi zao zote na makampuni yao ya ulinzi yaliyoko Iraq. Zaidi ya televisheni kumi za nchini Iraq na vyombo vingine kadhaa vya habari vya Kiarabu na kimataifa vilianza kurusha matangazo ya moja kwa moja kuhusu maandamano ya mamilioni ya Wairaqi tangu mapema asubuhi na kusitisha matangazo yao ya kawaida.

Tarehe 5 mwezi huu wa Januari Bunge la Iraq lilipasisha azimio la kufukuza vikosi vya majeshi ya nchi za kigeni hususan Marekani katika ardhi ya Iraq. Uamuzi huo wa Bunge la Iraq ulichukuliwa baada ya jeshi la Marekani kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis aliyekuwa afisa wa wapiganaji wa kujitolea wa harakati ya al Hashdul Shaabi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.

/3873805

captcha