IQNA

17:12 - February 01, 2020
News ID: 3472428
TEHRAN (IQNA) – Watetezi wa haki za wahamiaji na haki za binadamu wamemlaani Rais Donald Trump wa Marekani kwa kupanua marufuku ya nchi ambazo raia wake wanakabiliwa na vizingiti vya uhamiaji kuingia nchini humo, hatua ambayo imetajwa kuwa na ajenda ya chuki dhidi ya raia wa kigeni.

Serikali ya Marekani Ijumaa imetangaza kuwa imewawekea vizingiti wasafiri wanaokusudia kuingia nchini humo kutoka Tanzania na nchi zingine tano.

Kwa mujibu wa taarifa wahajiri kutoka Myanmar (Burma), Eritrea, Kyrgyzstan na Nigeria watazuiwa kuingia Marekai kwa visa za uhamiaji. Raia wa Sudan na Tanzania nao hawataruhusiwa kushiriki katika ule mchakato wa bahati nasibu maarufu kama green card lottery ambapo wenye kufanikiwa huweza hatimaye kupata uraia wa Marekani.

Nchi hizo mpya zinaingia katika kundi la nchi nyingine saba ambazo raia wake walipigwa marufuku kuingia Marekani toka mwaka 2017. Nchi hizo, nyingi ni za raia wengi Waislamu ambazo ni Libya, Iran, Somalia, Syria, Yemen na pia nchi zisizokuwa za Kiislamu ambazo ni mahasimu wakubwa wa Marekani yaani Venezuela na Korea Kaskazini.

Tanzania imeingizwa katika orodha hiyo masaa machache baada ya utawala wa Trump kumpiga marufuku mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuingia nchini humo kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Makonda amezikasirisha nchi za Magharibi na hasa Marekani kutokana na vita vyake dhidi ya ushoga au uhusiano wa watu wa jinsia moja, ukahaba na dawa za kulevya mjini Dar es Salaam.

Mashirika ya kutetea haki za wahamiaji yamekosoa vikali sera hiyo ya Marekani na kusema: "Utawala wa Trump unaendelea kutekeelza ile ajenda ya itikadi kuwa wazungu ni wanadamu bora zaidi sambamba na kuwabagua watu kwa msingi wa dini na utaifa."

"Baada ya kuwabagua Waislamu, hivi sasa Trump anapanua zaidi sera zake kwa jamii zingine zisizokuwa za wazungu. Utawala wa Trump unaendelea kutumia sheria za uhamiaji kusongeza mbele ajenda yake ya chuki dhidi ya wageni," amesema Javeria Jamil, wakili katika Taasisi ya Kutetea Haki za Kiraia na Kiusalama za Wamarekani Wenye Asili ya Asia.

Naye Omar Jadwat wa Jumuiya ya Uhuru wa Kiraia Marekani amesema Trump amepanua zaidi sera zake za kuwazuia wahamiaji kutoka nchi za Waislamu kuingia nchini humo na sasa watu wa jamii zingine nao pia wanalengwa.

3470490

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: