IQNA

16:36 - February 03, 2020
News ID: 3472435
TEHRAN (IQNA) - Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zimepinga mpango wa 'muamala wa karne' uliopendekezwa na Marekani ambao unakandamiza haki za taifa la Palestina.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama wa OIC wamekutana leo katika mkutano wao wa dharura mjini Jeddah, Saudi Arabia baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuzindua mpango wake wa eti muamala wa karne kuhusu kadhia ya Palestina pamoja na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.

Akizungumza katika mkutano huo, Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina amesema kuwa, Muamala wa Karne umepasishwa na utawala wa Trump na utawala haramu wa Israel na Wapalestina hawakuwa sehemu ya mpango huo.

Azimio ambalo limepitishwa na OIC kupinga 'muamala wa karne' limependekezwa na Palestina na limepitishwa kwa wingi wa kura. "OIC inasisitiza msimamo wake wa kimsingi wa kuunga mkono taifa la Palestina katika mapambano ya kupata haki zake za kisheria ikiwa ni pamoja na kuanzishwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds (Jerusalem) mashariki."

Mkutano huo wa OIC umefanyika katika hali ambayo, Saudi Arabia imekataa kutoa visa kwa ujumbe wa Iran ambao ulipaswa kushiriki katika mkutano huo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Abbas Mousavi amesema Iran imewasilisha malalamiko rasmi kwa OIC ikilaani hatua ya Saudi Arabia kutumia vibaya uwenyeji wake wa  jumuiya hiyo.

Viongozi wa Iran wametangaza bayana kupinga mpango huo wa Trump na kuutaja kuwa ni wenye kuwadhalilisha Wapalestina na kuwapokonya haki zao kwa maslahi ya utawala bandia wa Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba kile kinachotajwa kuwa 'Muamala wa Karne' kwa hakika ni 'Hiana na Usaliti' dhidi ya taifa la Palestina.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa mpango huu wa Rais Donald Trump wa Marekani unapingana na hati ya Umoja wa Mataifa na vilevile maazimio ya Baraza la Usalama la umoja wa huo kuhusiana na Palestina. Mpango huo ambao ni muamala baina ya Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na hauutambui upande wa Palestina ambao ndio mmiliki halisi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ni muamala wa kisiasa wenye lengo la kuwaokoa wanasiasa hao wawili wanaokabiliwa na kashfa na migogoro mingi ya ndani.

3876168

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: