IQNA

Balozi wa Syria: Umoja wa Mataifa umefeli kuishinikiza Israel kuhusu Palestina, Syria

19:29 - April 24, 2020
Habari ID: 3472699
TEHRAN (IQNA) - Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema Baraza la Usalama la umoja huo limefeli kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel utekeleza maazimio ya baraza hilo kuhusu Palestina na Syria.

Akizungumza kwa njia ya video katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), Bashar al-Ja'afari, Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema Baraza la Usalama limeshindwa kuuchukulia hatua utawala ghasibu wa Israel kutokana na mashinikizo ya baadhi ya wanachama wa kudumu wa baraza hilo.

Amesema kati ya maazimio ambayo Umoja wa Mataifa umeshindwa kutekeleza ni maazimio nambari 242, 338 na 497 kuhusu ardhi za Waarabu zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Maazimio hayo yanataka utawala ghasibu  wa Israel uache kukalia kwa mabavu ardhi za Waarabu.

Al- Ja'afari amesisitiza kuwa Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Isrel ni sehemu isiyotenganika ya ardhi ya Syria na kuongeza kuwa, kusitishwa ukaliwaji mabavu eneo hilo la kistratijia ni kipaumbele cha serikali ya Syria.

AIdha amesema hatua ya Umoja wa Mataifa kutofuatilia utekelezwaji wa maazimio hayo ni jambo ambalo limezichochea nchi zingine duniani kuacha kutekeleza majukumu ya kisheria na kubadilisha ukweli wa mambo na mfano ni ile hatua ya kichokozi ya Marekani ya kutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel mwezi Disemba 2017 na baada ya hapo kutambulia 'umiliki' wa Israel wa Miinuko ya Golan mnamo Machi 2019.

Al-Ja'afari amesema Syria na aghalabu ya nchi dunaini zinalaani hatua kama hizo za upande mmoja za Marekani kwani Washington haina haki ya kisiasa, kimaadili au kisheria kuamua hatima ya nchi zingine. Aidha amekosoa hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukiuka mara kwa mara anga ya Lebanon kwa kuvurumisha makombora ya kuilenga Syria kupitia anga ya nchi hiyo. Amesema mashambulizi kama haya yanakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa na yanalenga kuwaunga mkono magaidi wachache wakufurishaji wanaopata himaya ya kigeni nchini Syria.

3471238

captcha