IQNA

Muungano ambao natija yake imekuwa ni hitilafu

11:19 - February 19, 2020
Habari ID: 3472486
TEHRAN (IQNA) - Huku vita dhidi ya Yemen vikikaribia kutimiza mwaka wake wa tano, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE au Imarati) ambayo inaunda muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia imo mbioni kuondoa majeshi yake yote katika nchi hiyo.

Katika vita dhidi ya Yemen, wanajeshi wasiopungua 180 wa Imarati wameuawa. Mbali na hasara hiyo, Imarati imekabiliwa na tishio kubwa kutoka kwa wapiganaji wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah na jeshi la Yemen. Vitisho hivyo ambavyo katika mwaka uliopita wa 2019 viliongezeka, vinatajwa na wajuzi wa mambo kuwa, viimeifanya Imarati ichukue uamuzi wa kujiondoa katika vita huko Yemen.

Katika hatua ya awali kwenye msimu wa joto wa mwaka uliopita wa 2019, Imarati ilipunguza wanajeshi wake huko Yemen na waliobakia wakawa na jukumu la kutoa mafunzo kwa mamluki. Katika hatua ya pili, wanajeshi wa Imarati waliokuwa wamebakia sasa wanaondoka wote.

Hata hivyo uwepo wa Imarati katika vita hivyo haujafikia tamati, kwani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Abu Dhabi iliandaa askari wazawa na kuwapatia mafunzo ambao kimsingi wanapigana kwa niaba ya Imarati. Baraza la Mpito la Kusini na al-Hizam al-Amni ni vikosi muhimu vyenye mfungamano na Imarati vilivyoko kusini mwa Yemen. 

Kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Imarati kutoka Yemen kuna jumbe na risala mbili muhimu. Ujumbe wa kwanza ni kuwa, makubaliano ya Riyadh yaliyotiwa saini Novemba mwaka jana kwa upatanishi wa Riyadh baina ya Baraza la Mpito la Kusini na serikali iliyojizulu ya Rais Mansur Hadi kivitendo yamevunjika; jambo ambalo alilikiri bayana hivi karibuni msemaji wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen.

Ujumbe wa pili ni kuwa, kuondoka kikamilifu Imarati katika vita huko Yemen kuna maana ya kusambaratika kikamilifu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, jambo ambalo limeashiria pia na gazeti la Rai al-Youm na kuitaja hatua hiyo kama mwanzo wa kumalizika vita nchini Yemen, kufikia tamati pia ushirika wa Saudia na Imarati na kuparaganyika 'Muungano wa Kiarabu".

Ukweli wa mambo ni kuwa, Imarati imefikia natija hii kwamba, wanaoendesha vita dhidi ya Yemen hawatapa ushindi. Kuendelea vita sambamba na kuhesabiwa kuwa ni pigo na kushindwa kisiasa na kijeshi, kutakuwa na gharama kubwa zaidi kiuchumi.

Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilitahadharisha katika ripoti yake mwishoni mwa mwaka uliopita kuhusiana na hali ya kiuchumi ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Filihali, baada ya kujiondoa kikamilifu Imarati katika vita huko Yemen, mpira sasa uko katika uwanja wa Saudia ambayo inapaswa kuamua kuhusu kuhitimisha vita katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

3879695

captcha