IQNA

Misikiti yote ya Iran kufunguliwa kwa ajili ya swala zote

0:09 - May 31, 2020
Habari ID: 3472820
TEHRAN (IQNA) – Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema misikiti yote nchini itafunguliwa kwa ajili ya swala zote.

Akizungumza Jumamosi mjini Tehran katika mkutano wa Idara Kitaifa ya Kupambana na COVID-19,  Rais Rouhani amesema idara hiyo imechukua uamuzi wa kuidhinisha misikiti yote ifunguliwe kote Iran. Hatahivyo amesisitiza kuwa Waumini watakaoingia misikitini watatakiwa kufuata taratibu na kanuni zote za kiafya zilizowekwa ili kuzuia kuenea ugonjwa ambukizi wa COVID-19. Kati ya masharti ya kuzingatiwa katika misikiti ni watu kutokaribiana katika safu za swala.

Iran ilifunga misikiti yake mwezi Machi kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19 na mapema mwezi Mei misikiti ilifunguliwa katika baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na maambukizi madogo sana ya COVID-19. Aidha swala ya Idul Fitr iliswaliwa katika baadhi ya misikiti na viwanja na mabustani kwa kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya.

Wakuu wa afya nchini Iran wanasema sasa wameweza kudhibiti kasi ya maambukizi ya COVID-19 na kwa msingi huo vizingiti mbali mbali vilivyokuwa vimewekwa vimeanza kupunguzwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Iran hadi kufikia Mei 30, watu 148,950 walikuwa wameambukizwa COVID-19 nchini Iran na miongoni mwaka 116,817 wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata matibabu hospitalini.  Aidha kwa mujibu wa takwimu hizo hadi sasa watu 7,734 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini.

3901897

captcha