IQNA

18:23 - June 02, 2020
News ID: 3472829
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, watawala wa Marekani ni watuhumiwa wa kuvunja haki za kimsingi kabisa za binadamu na inabidi wapandishwe kizimbani kwenye mahakama za kimataifa.

Hujjatul Islam wal Muslimin Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo Jumanne hapa mjini Tehran na huku akigusia machafuko yanayoendelea katika kona zote za Marekani amesema, ukatili uliofanywa na jeshi la polisi la Marekani dhidi ya Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika, ndiyo picha halisi ya Marekani.

Mkuu huyo wa Idara ya Mahakama ya Iran pia amesema, wale wanaodai ni watetezi wa haki za binadamu wamenyamaza kimya mbele ya ukandamizaji wa haki za kimsingi kabisa za kibinadamu duniani na kuongeza kuwa, suala hapa haliwahusu Wamarekani wasio wazungu tu, bali ubaguzi wa rangi ni kitu kilichokita mizizi nchini Marekani.

Jumatatu wiki iliyopita, katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota na polisi mzungu kwa jila la Derek Chauvin alimuua kikatili Mmarekani mweusi George Floyd, jambo ambalo limeibua maandamano makubwa ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena nchini Marekani, kwa lengo la kulaani ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo. Polisi huyo mzungu alifanya kitendo cha kinyama kwa kubana shingo na kumyima pumzi taratibu Floyd, hadi alipoaga dunia, kwa kutumia goti la mguu wake wa kushoto, tena akiwa ametulia kabisa bila ya kuwa na wasiwasi wowote. Baada ya kukamatwa na kutuhumiwa kwa mauaji ya daraja ya tatu hapo tarehe 29 Mei, hatimaye Chauvin aliachiliwa huru kwa dhamana ya dola laki tano.

Sasa badala ya rais wa Marekani kutafakari namna ya kutatua tatizo hilo, ametoa vitisho dhidi ya waandamanaji. Mapema siku ya Ijumaa, Donald Trump aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kuwataja waandamanaji wanaolalamikia mauaji ya Mmarekani mweusi kuwa ni magenge ya wahuni na wahalifu. Si hayo tu lakini vile vile ametangaza serikali ya kijeshi na kutishia kuwapiga risasi waandamanaji. Katika sehemu moja ya ujumbe wake aliandika: "Pamoja na matatizo yote yaliyopo hivi sasa, tutaweza kudhibiti hali ya mambo. Iwapo uasi na uporaji wa maduka utaanza, wafanya fujo watafyatuliwa risasi."

Ubaguzi wa rangi na matumizi ya mabavu dhidi ya wale wanaotajwa kuwa watu wa rangi nchini Marekani na hasa weusi, ni jambo lenye historia ndefu nchini humo. Licha ya mapambano ya muda mrefu ya weusi kwa ajili ya kutetea haki zao, lakini wangali ni wahanga wakubwa wa ubaguzi na matumizi ya mabavu na hasa kutoka kwa polisi ya nchi hiyo.

3902419

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: