IQNA

Katika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi

Waandamanaji Marekani wavunja masanamu ya Christopher Columbus

12:20 - June 12, 2020
Habari ID: 3472858
TEHRAN (IQNA) - Waandamanaji wenye hasira nchini Marekani wanaendeleza mkakati wa kuanugusha, kuharibu ama kuondoa masanambu ya wabaguzi wa rangi hasa Christopher Columbus.

Katika miji mbali mbali ya Marekani  waandamanaji wamebomoa masanamu ikiwa ni pamoja na sanamu la Christopher Columbus, mzungu kutoka Ulaya aliyedai kuvumbua bara Amerika na sanamu ya Edward Colston aliyekuwa mfanyabiashara wa watumwa, katika karne ya 17.

Waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani  wamebomoa, kuharibu na kuvunja vichwa vya sanamu ya Christopher Columbus kuanzia miji ya Boston upande wa kaskazini hadi Miami huko kusini.

Katika tukio la hivi karibuni kabisa, sanamu la Columbus limebomolewa Alhamisi katika mji wa Camden, jimboni New Jersey. Baraza la mji huo limesema linaangalia upya nembo hizo ambazo zinaashiria ubaguzi wa rangi.

Wanasiasa mbali mbali nchini Marekani wametoa wito wa kuondolewa alama zote zinazowakilisha wakoloni na wamiliki watumwa baada ya maandamano yaliochochewa na kifo cha George Floyd wiki tatu zilizopita.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi ametaka kuondolewa kwa sanamu kubwa 11 za wanajeshi na maafisa wa enzi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani mwaka 1861 hadi 1865.

Hatahivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amekaidi pendekezo hilo na kusisitiza kwamba hatofikiria kubadilisha majina ya kambi za kijeshi ambazo zimepewa majina ya majenerali wabaguzi wa rangi na ambao waliunga mkono utumwa.

Mnamo Mei 25, afisa wa polisi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota nchini Marekani alimbinya shingo kwa kutumia goti kwa dakika 9 hivi George Floyd, Mmarekani mweusi mwenye asili ya Afrika hadi akakata roho.

Mauaji hayo ya kinyama yaliibua maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa Marekani kupinga ubaguzi wa rangi huku miito ikitolewa ya kulifanyia marekebisho jeshi la polisi na kuondolewa nembo zote za ubaguzi wa rangi nchini humo.

Christopher Columbus  alikuwa baharia wa Kiitalia ambaye aliongoza mabahari kadhaa waliofika bara Amerika karibu miaka 530. Baada ya Columbus kuingia bara Amerika ulianza ukoloni wa madola ya Ulaya katika bara hilo na ukoloni huo uliandamana na ukatili mkubwa dhidi ya wenyeji wa bara hilo waliopokonywa ardhi zao na kuangamizwa kwa umati sambamba na kuanza biashara ya kikatili ya utumwa. Wakoloni makatili wazungu waliwasafirisha watumwa kutoka Afrika kwa ajili ya kuwafanyisha kazi katika mashamba ya bara Amerika.

2738252

captcha