Rais Rouhani aliyasema hayo mapema leo Jumanne alipohutubia halaiki kubwa ya watu katika mkoa wa Semnan mashariki mwa Iran na kubaini kuwa: "Taifa la Iran limepata mshindi mbele ya mashinikizo yote ya vikwazo na matatizo ya kieneo na kimataifa."
Rais Rouhani amegusia makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1 sambamba na utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia maarufu kama Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kuongeza kuwa: "JCPOA ni fakhari ya kisiasa na kisheria kwa watu wa Iran."
Rais wa Iran amesema kufuatia mapatano hayo, maazimio sita ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mengine 12 ya Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA dhidi ya Iran yameondolewa.
Aidha amekosoa wale wanaodai kuwa taifa la Iran halijapata ushindi na kwamba Marekani ndie mshindi katika mapatano ya nyuklia.
Rais Rouhani amesema vikwazo vimeondolewa na uhusiano na Iran na benki za dunia unafunguliwa hatua kwa hatua. Amesema wafanya biashara wa Iran wanaweza kuuza bidhaa nje lakini amesema itachukua muda wawekezaji wa kigeni kuja Iran.