IQNA

Rais Rouhani akihutubu bungeni

Iran itakabiliana na Marekani ikikuka mapatano ya nyuklia

11:55 - December 05, 2016
Habari ID: 3470719
IQNA-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran litachukua hatua madhubuti na za kivitendo mkabala na uvunjaji ahadi, kigugumizi na ucheleweshaji wa aina yoyote ile katika kutekeleza mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Rais Hassan Rouhani amesema hayo Jumapili katika hotuba yake kwenye Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, na kubainisha kwamba, Iran haitakiuka makubaliano ya nyuklia lakini wakati huo huo amesisitiza kuwa taifa hili litatoa jibu kali kwa ukiukaji wa makubaliano ya nyuklia kwani muswada uliopasishwa hivi karibuni katika Bunge la Marekani ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano hayo.

Rais Rouhani amebainisha kuwa, Rais wa Marekani anapaswa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa kutumia mamlaka aliyonayo azuie utekelezwaji kivitendo vikwazo vilivyoongezewa muda dhidi ya Iran.

Rais Hassan Rouhani ameongeza kuwa, Iran inatambua kuwa, suala la kupanua ushirikiano wake kimataifa ni haki yake hivyo haina haja ya kuiomba ruhusa nchi fulani kuhusiana na jambo hilo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Bunge la Iran Jumapili liliaani hatua ya wajumbe wa Bunge la Kongresi nchini Marekani kurefusha kwa muda wa miaka 10 sheria ya kuiwekea Iran vikwazo na wametoa wito wa kuchukuliwa hatua thabiti za kukabiliana na uhasama huo wa Bunge la Marekani.

Muswada wa kurefusha muda wa vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi ulipasishwa kwa kura 99 za ndio bila ya kuweko kura yoyote ya kupinga katika Baraza la Sanate la Marekani Alkhamisi iliyopita.

Tarehe 16 Januari mwaka huu, Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumaini, zilianza utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA ambayo yalitiwa saini tarehe 14 Julai, 2015. Mazungumzo kuhusu mapatano hayo yalisimamiwa na Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Iran ilikubali kuwekea mipaka fulani miradi yake ya nyuklia na upande wa pili nao ukaahidi kuondoa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa Iran kutokana na miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani.

Iran inatekeleza ahadi zake zote kwa mujibu wa mapatanoKwa mujibu wa ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zilizoungwa mkono pia na mataifa mengine yaliyotia saini makubaliano hayo yanayojulikana kwa jina la JCPOA, hadi hivi sasa Iran imetekeleza kikamilifu ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo. Hatahivyo Marekani imeonyesha wazi kuwa haina nia ya kutekeleza ahadi zake.

3550713

captcha