IQNA

Wananchi wa Syria washiriki katika uchaguzi wa bunge

18:08 - July 19, 2020
Habari ID: 3472979
TEHRAN (IQNA) - Wananchi wa Syria leo wanapiga kura kwa ajili ya kuwachagua wawakilishi wao wa bunge la kitaifa.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema saa moja asubuhi kwa saa za Syria na vitaendelea kuwa wazi hadi saa moja usiku na kutakuwa na uwezekano wa muda kuongezwa kulingana na jinsi zoezi hilo litakavyofanyika.

Wagombea 1,656 wakiwemo wanawake 200 wanachuana katika uchaguzi huo kuwania viti 250 vya Bunge la nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Syria kila mwananchi wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 18 anaweza kupiga kura kama ambavyo kwa mujibu wa sheria wanajeshi na polisi wanaweza kupiga kura.

Kampeni za uchaguzi huo zilikamilika rasmi hapo jana. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, kampeni za uchaguzi zinapaswa kufikia ukingoni saa 24 kabla ya kufanyika uchaguzi na hakuna mgombea ambaye anaruhusiwa kufanya kampeni baada ya muda huo.

Tume ya Uchaguzi wa Syria imetangaza kuwa, kumetengwa vituo 7,277 vya kupigia kura kote nchini humo. Uchaguzi wa leo wa Bunge nchini Syria unafanyika baada ya kuakhirishwa mara mbili kutokana na kuenea virusi vya Corona.

Syria ilitumbukia katika mgogoro mwaka 2011 kufuatia hujuma kubwa ya makundi ya kigaidi chini ya uungaji mkono wa Saudia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadili mlingano katika eneo kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni; njama ambazo hazikufanikiwa.

3472033

captcha