IQNA

Israel yashambulia Doha kuwalenga viongozi wa Hamas

11:28 - September 10, 2025
Habari ID: 3481212
IQNA-Ndege za kivita za Israel zimetekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya makao makuu ya harakati za upinzani za Hamas katika mji mkuu wa Qatar, Doha, katika kile vyombo vya habari vya Israel vilikitaja kama “operesheni ya mauaji ya kisiasa.”

Mashambulizi hayo yalifanyika wakati viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, walipokuwa wamekutana kujadili pendekezo jipya la Marekani kuhusu kusitisha mapigano huko Gaza.

Jeshi la Israel lilitoa taarifa likithibitisha kuwa lilitekeleza kile lilichokiita “shambulizi sahihi” lililolenga uongozi wa juu wa Hamas.

Afisa mmoja mwandamizi wa utawala wa Israel aliiambia Channel 13 ya Israel kuwa Khalil al-Hayya, kiongozi wa Hamas, pamoja na Zaher Jabarin, mwenyekiti wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas katika Ukingo wa Magharibi, walikuwepo kwenye kikao hicho kilicholengwa.

Ripoti pia zilidokeza kuwa Khaled Mashaal, kiongozi wa muda mrefu wa Hamas ambaye Israel ilijaribu kumuua nchini Jordan mwaka 1997, alihudhuria kikao hicho.

Hamas yasema viongozi wake wa juu wamenusurika

Baadaye, Hamas ilitoa taarifa kali ya kulaani jaribio la Israel la kuwaua wajumbe wake wa mazungumzo waliokuwa Doha. Kundi hilo la Kipalestina lililitaja shambulizi hilo kama “jinai ya kuchukiza” na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Hamas ilithibitisha kuwa wajumbe wake wa juu walinusurika, lakini wanachama watano wa kundi hilo waliuawa shahidi, akiwemo Jihad Labad, mkurugenzi wa ofisi ya Khalil al-Hayya; Hammam al-Hayya, mwanawe Khalil; Abdullah Abdul Wahid, Moumen Hassouna, na Ahmed al-Mamlouk—wote wakielezewa kama wasaidizi wa ujumbe huo.

Aidha Badr Saad Muhammad Al-Humaidi, afisa wa usalama wa Qatar, aliuawa shahidi katika hujuma hiyo.

Hamas imesema kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anajaribu kuvuruga juhudi za amani, na pia imeilaumu serikali ya Trump kwa kuunga mkono ugaidi wa Israel.

Taarifa hiyo ilisema kuwa shambulizi hilo linaonesha tena kuwa Israel ni tishio kwa utulivu wa kikanda na wa kimataifa, na inaendeleza sera za kuhamisha na kuharibu maisha ya Wapalestina.

Hamas ilisisitiza kuwa, "kusitishwa mara moja kwa vita vya mauaji ya halaiki, kuondoka kabisa kwa majeshi ya Israel kutoka Gaza, kubadilishana wafungwa kwa haki, na msaada wa ujenzi upya wa Gaza."

Kundi hilo lilithibitisha tena dhamira yake ya kuendeleza mapambano na lengo la kuanzisha taifa huru la Palestina lenye mji wa al-Quds kama mji mkuu wake.

Qatar yalaani ‘shambulizi la kiwoga’

Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ililaani “shambulizi la kiwoga la Israel” dhidi ya makao ya Hamas huko Doha, ikilitaja kama ukiukaji wa sheria za kimataifa na tishio kwa usalama wa Qatar.

“Dola ya Qatar inathibitisha kuwa haitavumilia hatua yoyote inayolenga usalama au mamlaka yake,” ilisema. “Uchunguzi unaendelea kwa kiwango cha juu kabisa, na maelezo zaidi yatatolewa mara yatakapopatikana.”

Shambulizi hilo lilifanyika siku mbili baada ya Rais Trump kuitaka Hamas ikubali pendekezo lake la kusitisha mapigano Gaza, akitoa kile alichokiita “onyo la mwisho” kwa kundi hilo la Kipalestina.

“Nimeionya Hamas kuhusu madhara ya kutokukubali. Hili ni onyo langu la mwisho, halitakuwepo lingine!” Trump aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social siku ya Jumapili.

Afisa mmoja wa Israel ambaye hakutajwa jina aliiambia Channel 12 ya Israel kuwa Rais Trump alitoa idhini ya mashambulizi hayo dhidi ya Doha.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, alithibitisha Jumanne kuwa utawala wake umekubali pendekezo jipya la Trump kuhusu kuachiliwa kwa mateka na kusitisha mapigano Gaza.

“Vita vya Gaza vinaweza kuisha kesho,” alisema waziri huyo katika mkutano wa waandishi wa habari nchini Croatia.

Hamas ilisema Jumapili kuwa imepokea “mawazo mapya” kutoka Marekani kupitia wapatanishi kuhusu jinsi ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano. Harakati hiyo ilisema iko tayari kuunga mkono juhudi zozote mpya za kukomesha uchokozi wa Israel.

3494551

captcha