IQNA

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Marekani haiwezi kutumia Utaratibu wa azimio 2231 la Baraza la Usalama la UN

22:14 - August 19, 2020
Habari ID: 3473084
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jitihada mpya za Marekani za kutumia azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kutoa pigo kwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA tayari zimeshafeli.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa: "Utaratibu wa azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  uko wazi kwamba ni 'pande husika katika JCPOA' ndizo zinazoweza kuutumia. Kwa kuzingatia kuwa Marekani imejiondoa katika JCPOA haiwezi tena kutumia utaratibu huo."

Rais Rouhani amesema pande zote katika JCPOA zinapaswa kulaani jitihada hizo za Marekani. Ameoneza kuwa, Marekani kwa mara nyingine imetengwa na taifa la Iran limebakia kuwa adhimu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria historia ndefu ya uhasama wa Waistikbari dhidi ya taifa la Iran na kusema:

"Wananchi na viongozi wa Iran kwa kusimama kidete na muqawama mbele ya njama za maadui, wameweza kuwafikishia ujumbe wakuu wa White House kuwa wamefanya kosa kuhusu Iran."

Halikadhalika amesema watawala majabari katika Ikulu ya White House na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran si mambo ya kudumu.

Rais Rouhani ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuuza nje ya nchi bidhaa zisizo za mafuta. Ameongeza kuwa,  hatua za Iran za kuhakikisha vikwazo haviidhuru nchini ni pigo kwa Marekani

 Baada ya Marekani kuumbuka vibaya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia kushindwa muswada wake dhidi ya Iran, Rais Donald Trump aliahidi kwamba, wiki hii atafanya juhudi za kuhakikisha anautumia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", kwa kimombo "Trigger Mechanism" kwa ajili ya kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Trump ambaye ni mkosoaji mkubwa wa makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA Mei 8 mwaka 2018 aliitoa nchi yake katika makubaliano hayo. 

3917567

captcha