IQNA

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akihutubu katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Zama za ubeberu zimefikia tamati, ni wakati wa walimwengu kusema "la" kwa ubabe na utumiaji mabavu

17:29 - September 23, 2020
Habari ID: 3473196
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani amesema: "Marekani haiwezi kutulazimisha kufanya mazungumzo wala kuanzisha vita dhidi yetu" na akasisitiza kwamba, sasa ni wakati wa walimwengu kusema "la" kwa ubabe na utumiaji mabavu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika hotuba aliyotoa kwa njia ya video kupitia mawasiliano ya intaneti katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Amesema, zama za ubeberu na mamlaka ya dola moja kutoa amri kwa madola mengine zimefikia tamati na akafafanua kuwa: Kutoa mara mbili Baraza la Usalama tamko la wazi la "hapana" kwa Marekani kwa sababu ya kutaka kulitumia kimaslahi na kinyume cha sheria baraza hilo na azimio nambari 2231 ni ushindi si kwa Iran tu bali kwa zama za mfumo wa kimataifa katika ulimwengu wa baada ya enzi za Magharibi ambapo utawala unaojinadi kuwa na mamlaka ya kuamuru unazama kwenye lindi la kutengwa ulilojichimbia wenyewe.

Rais Rouhani ameeleza pia kwamba "maisha katika hali ya vikwazo ni magumu, lakini gumu zaidi ya hilo ni kuishi bila kujitawala na kuwa huru." Ameongeza kuwa Iran, ambayo ndiyo yenye demokrasia kongwe zaidi katika Asia Magharibi, inajivunia mfumo wake wa utawala unaoendeshwa kwa ridhaa ya wananchi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake katika mkutano mkuu wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuna baadhi wanazungumzia haki za binadamu, lakini wanatumia mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa kulenga maisha, afya na hata uhai wa Wairani wote na akaongezea kwa kusema: Wao na vibaraka wao ndio wanaohusika moja kwa moja katika kuwasha moto wa vita, uchokozi na uvamizi huko Palestina, Afghanistan, Yemen, Syria, Iraq, Lebanon, Libya, Sudan na Somalia, lakini badala yake wanaitaja Iran kuwa ndio sababu ya kushindwa kwao kukabiliana na irada ya wananchi wa mataifa ya eneo.

Rais Rouhani amekumbusha pia kuwa, baadhi wanadai kwamba wamekuja katika eneo kwa ajili ya kupambana na Saddam ilhali wao ndio waliolijenga na kulitia nguvu nduli hilo katika vita dhidi ya Iran; na sasa pia wanajinasibu kuwa wanapambana na ugaidi na DAESH ilhali wao ndio waliolianzisha kundi hilo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia silaha zenye gharama ya mabilioni ya dola linazouziwa eneo la Asia Magharibi na kugeuzwa ghala la mada za miripuko na akabainisha kuwa, Marekani inatoa tuhuma za uongo dhidi ya Iran kwamba inataka kuunda silaha za nyuklia ilhali nchi hiyo peke yake ndiyo iliyoweka rekodi ya kufanya uhalifu wa kutumia silaha za nyuklia katika historia ya wanadamu na kisha unautumia utawala pekee wenye silaha hizo katika eneo la Asia Magharibi (Israel) kuviendesha na kuvichezesha vikaragosi vyake katika eneo hili.

3924753

captcha