IQNA

Hamas yapinga madai ya UAE kuhusu kusitishwa upanuzi wa vitongoji vya Wazayuni

20:18 - October 02, 2020
Habari ID: 3473222
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepinga madai ya afisa mwandamizi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa eti utawala bandia wa Israel umesitisha upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni baada ya utawala huo kuanzisha uhusiano na nchi mbili za Kiarabu za UAE na Bahrain.

Msemaji wa Hamas Hazem Qasim ametoa taarifa na kusema upanuzi usio na kikomo wa vitongozji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukiongo wa Magharibi ni jambo ambalo limeweka wazi madai yasiyo na msingi ya tawala za Kiarabu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE Sheikh Abdullah bin Zayed bin Sultan Al Nahyan amedai kuwa mapatano ya nchi yake na Israel yameulazimu utawala huo bandia kusitisha upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Wiki iliyopita, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilitangaza kuwa, Waziri Mkuu wa utawala huo haramu Benjamin Netanyahu ameafiki mpango wa kujengwa nyumba mpya elfu tano katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi.

Ripoti ya vyombo hivyo vya habari vya Kizayuni imeongeza kuwa, mnamo mwezi Februari mwaka huu Netanyahu alisitisha mpango huo wa ujenzi wa vitongoji kwa lengo la kuepusha hatua hiyo isije ikatibua makubaliano ya mapatano yaliyokuwa yamepangwa kusainiwa baina ya Israel na Imarati na Bahrain.

Hayo yanaripotiwa wakati UAE ilisikika ikidai mara kadhaa kwamba, kusitishwa mpango wa kulimega eneo la Ufukwe wa Magharibi na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni sehemu ya makubaliano ya mapatano kati yake na utawala haramu wa Israel.

Msemaji wa Hamas amebainisha kuwa, kupitishwa mradi wa ujenzi wa nyumba mpya katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kumekashifu na kuuanika hadharani uongo wa Waarabu wafanyamapatano.

/3472695

captcha