IQNA

Wapiga kura wa Algeria waunga mkono katiba mpya

16:42 - November 02, 2020
Habari ID: 3473321
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa Algeria wameunga mkono mabadiliko ya katiba katika kura ya maoni iliyofanyika Novemba mosi nchini humo.

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Algeria, Mohamed Charfi, amesema zaidi ya asilimia 66 ya wapiga kura wameunga mkono mabadiliko katika katiba. Kuhusu idadi ndogo ya wapiga kura, amesema watu wengi hawakujitokeza kupiga kura kutokana na hofu ya kuambukizwa corona. Ni takribani asilimia 15 tu ya wa wananchi walishiriki katika kura hiyo ya maoni. Awali tume ya uchaguzi ilikuwa imesema asilimia 24 ya waliotimiza vigiezo vya kupiga kura walikuwa wamejitokeza.

Kura hiyo ya maoni ilikuwa na lengo la kubadilisha katiba ambayo ni kati ya masalia ya utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika.

Ikumbukwe kuwa Bouteflika aliondoka madarakni Aprili 2019 kufuatia maandamano makubwa ya wananchi waliokuwa wanataka mabadiliko. Nafasi yake ilichukuliwa na  Abdelmadjid Tebboune, mwenye umri wa miaka 75, ambaye amechukua hatua kadhaa za kuleta mabadiliko katika muundo wa kisiasa nchini humo. Ili kuwavutia wapinzani  Rais Tebboune, aliahidi kuwa hatua yake muhimu ya marekebisho itakuwa ni kufanya mabadiliko muhimu na ya kimsingi katika katiba ya Algeria.

Kati ya malengo ya kuandikwa katiba mpya Algeria ni kuzuia nchi hiyo kurejea katika zama za utawala wa kidikteta wa mtu mmoja. Kwa msingi huo katiba mpya inabana muhula wa urais kuwa ni mihula miwili tu. Aidha katiba mpya inalenga kumpunguzia rais mamaka na kulipa bunge uwezo zaidi na pia kuvipa vyombo vya mahakama uhuru wa utendaji kazi. Halikadhalika katiba mpya inalenga kuwapa wananchi uhuru zaidi wa maoni na kujieleza.

Pamoja na hayo,  kumekuwa na mjadala mkubwa  kuhusu mabadiliko ya katiba ya Algeria. Vyama vingi vya kisiasa vimepinga kufanyika kura ya maoni wakati huu.  Wapinzani wanaamini kuwa kura ya maoni iliyofanyika ilikuwa hatua ya kimaonyesho tu.

Lakini waungaji mkono wa mabadiliko ya katiba na kura ya maoni wanasema matukio ya kisiasa Algeria katika mwaka mmoja uliopita yalikuwa ni ya kurudhisha na kwamba nchi hiyo sasa imeingia katika duru mpya ya uhai wake wa kisiasa katika kile ambacho wanakitaja kuwa ni 'Jamhuri ya Tano."

Aidha waungaji mkono wa kura ya maoni wanaamini kuwa, katiba mpya itahitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo wapinzani wanasema katiba mpya iliyopigiwa kura haitaweza kuleta mabadiliko ya kimsingi nchini humo bali kile kitakachofanyika ni kuzaliwa upya mfumo uliopita wa kisiasa.  Rais  Abdelmadjid Tebboune, amedai kuwa, katiba mpya itaweka msingi imara ya mabadiliko katika nchi hiyo.

3473014

captcha