IQNA

Maombolezo ya Bibi Maasuma SA

21:05 - November 26, 2020
Habari ID: 3473397
Siku kama ya leo miaka 1241 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Musa bin Jaafar A.S mmoja wa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu. Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha AS kuwasili Khorassan nchini Iran, Bibi Maasuma alichukua uamuzi wa kuondoka Madina na kumfuata kaka yake huko Khorassan, lakini akiwa njiani aliamua kusimama katika mji wa Qum.

Baada ya kupumzika katika mji mtakatifu wa Qum kwa muda wa siku 17 hatimaye bibi huyo mtukufu aliaga dunia kutokana na maradhi, au kama wanavyosema baadhi ya wanahistoria, kutokana na sumu aliyopewa. Bibi Maasuma A.S amezikwa katika mji huo mtukufu.

Sadiqa

Weledi wakubwa wa kidini walimtaja Hadhrat Maasuma kwa lakabu ambayo iliashiria cheo chake cha juu cha kielimu, kimaadili na kimaanawi.  Lakabu kama vile 'Sadiqa' ambayo inamaanisha mwanamke msema kweli sana au lakabu ya  'Muhaditha'  yaani mwanamke  mwenye kufikisha au kusimulia hadithi.  Alikuwa akinukulu hadhiti kutoka kwa baba yake na babu zake watukufu.

Jina la 'Fatima Binti Musa bin Jaafar' limeonekana katika silisila ya baadhi ya riwaya ambapo Maulamaa wa Kishia na Ahli Sunna wamenukulu na kuzikubali riwaya alizoziwasilisha kutokana na kuwa ziliweza kuthibitika na pia zilikuwa sahihi. Kati ya riwaya hizi ni zile zinazonasibishwa na Bibi Fatima Zahra AS na Mtume SAW.  Hadithi hizo ni 'Hadithi ya Ghadir' na 'Hadithi ya Manzilat' kuhusu nafasi ya Imam Ali AS. Katika hadithi hii, Mtume SAW alijinasibisha na Imam Ali AS na kusema nasaba hii ni kama ile ya Harun na Musa AS.

Hali kadhalika Hadhrat Maasuma SA katika kubainisha tukio muhimu la Ghadir, alifafanua kuhusu hadhi na cheo cha juu cha Ahul Bayt wa Mtume SAW ili watu wasighafilike na kile ambacho waliachiwa na Rasulullah SAW.

Karima wa Ahul Bayt

Kwa mujibu wa riwaya mbali mbali, Hadhrat Maasuma SAW alikuwa na lakabu nyingine mashuhuri ya 'Karima Ahlul Bait'. 'Karima' ni neno lenye maana ya mwanamke mkarimu na mrehemevu. Hadhrat Maasuma SAW alipitisha maisha yake yaliyojaa saada akiwa anajishughulisha na kutoa mafunzi ya Kiislamu na kuifasiri Qur'ani. Aidha alitumia wakati wake wote akijikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kutokana na mwenendo wake huu wa kufuata dini kikamilifu na kutotoka katika mkondo wa uongozi aliweza kufika daraja ya juu ya ukamilifu na ubora wa mwanaadamu. Imam Ridha AS katika kubainisha takuwa ya juu pamoja na utakasifu wa dada yake alimtaja kuwa ni 'Maasuma' yaani mwanamke aliyetakasika na asiyekuwa na dhambi.

3473234/

captcha