Akizungumza na IQNA wakati wa maadhimisho ya miaka mia moja tangu kuanzishwa upya kwa Hawza ya Qum (Hawza ‘Ilmiyya Qum), Ayatullah Arafi alisema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, seminari zimepitia "mabadiliko ya msingi katika elimu ya Qur'ani na tafsiri zake."
Aliongeza, “Shughuli za Qur'ani katika hawza zinahusisha maeneo makuu ishirini, na kueleza yote kungehitaji muda mrefu zaidi. Hapa nitataja kwa kifupi baadhi tu ya maeneo hayo.”
Miongoni mwa maeneo hayo, Ayatullah Arafi alielezea kuanzishwa kwa takriban majarida maalumu kumi yanayohusiana na Qur'ani, pamoja na programu zaidi ya ishirini za kitaaluma zinazolenga masomo ya Qur'ani na tafsiri. “Zaidi ya tafsiri kumi kamili za Qur'ani zimeandikwa na wanazuoni wa juu wa kidini,” alibainisha.
Alisisitiza pia juhudi kubwa za kutafsiri Qur'ani Tukufu kwa lugha mbalimbali, akisema kuwa “tafsiri nyingi pamoja na maelfu ya makala za kielimu zimeandaliwa.”
Ayatullah Arafi alieleza pia kuwa hawza sasa inaelekea kuunganisha tafsiri ya Qur'ani na fani za sayansi jamii na sayansi ya kibinadamu, akisema: “Tafsiri maalumu katika maeneo haya zimeanzishwa,” na kuongeza kuwa kazi mbalimbali za tafsir zimechapishwa kwa lugha tofauti.
Seminari ya Qum, inayojulikana kama Hawza ‘Ilmiyya Qum, ni miongoni mwa vituo mashuhuri zaidi vya elimu ya Kiislamu ya Kishia duniani. Ilianzishwa upya mwaka 1922, na imekuwa kitovu muhimu cha elimu ya dini, fiqhi, na fikra za Kiislamu nchini Iran na duniani kote.
Ikiwa katika mji mtakatifu wa Qum, kitovu cha elimu na ibada, Hawza ina mamia ya maelfu ya wanafunzi kutoka pande zote za dunia. Katika kipindi cha karne moja iliyopita, imetoa mchango mkubwa katika kuunda mwelekeo wa kielimu wa Kiislamu wa kisasa, kulea viongozi wa dini, na kuchangia pakubwa katika tafsiri na elimu ya Qur'ani na Hadithi.
3493055