IQNA

12:22 - May 08, 2022
Habari ID: 3475222
QOM (IQNA)- Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Iran Mh. Joshua Gatimu ametembelea Haram Takatifu ya Bibi Maasuma - Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-katika mji wa Qum.

Katika ziara hiyo Jumamosi, Balozi Gatimu na ujumbe alioandamana nao wamefahamishwa kuhusu maisha ya Bibi Maasuma. Ujumbe huo ambao ulijumuisha maafisa wa Ubalozi wa Kenya mjini Tehran umetembelea maeneo mbali mbali ya Haram Takatifu ya Bibi Masumah SA na kufahamishwa kuhusu hostoria na usanifu majengo wa eneo hilo takatifu.

Aidha wamebainishwa nafasi ya Bibi Maasuma mjini Qum na nafasi yake katika Kuanzishwa Chuo cha Kiislamu cha Qum na pia namna alivyoathiri Mapinduzi ya Kiislamu.

Mwanadiplomasia huyo wa Kenya alitunukiwa zawadi ya Qur'ani Tukufu yenye tarjuma ya Kiingereza. Halikadhalika ujumbe huo wa Kenya ulikuwa na kikao na wataalamu wa kidini ambao walijibu masuala na kutoa maelezo kuhusu Uislamu na Madhehebu ya Shia.

Ikumbukwe kuwa Bibi Fatima Maasuma SA, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim AS alizaliwa mwaka 173 Hijria Qamaria  katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu. Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha AS kuwasili Khorasan nchini Iran baada ya kubaidishwa na watawala wa kiimla wa wakati huo, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake,

Takribani miaka 1243 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria Bibi Fatma Maasuma aliwasili katika mji wa Qum, Iran.

Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba.

Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW).

Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria Qamari, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake Imam Ridha AS, Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa.

Alizikwa katika mji wa Qum na hii eneo alimozikwa BibI  Fatma Maasuma AS mjini Qum ni haram takatifu na ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu na maeneo mengine duniani, Waislamu na wasiokuwa Waislamu huenda kufanya ziara katika eneo hilo takatifu.

Kishikizo: joshua gatmu ، kenya ، maasuma ، qum ، waislamu ، bibi maasuma
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: