IQNA

11:19 - July 15, 2018
News ID: 3471595
TEHRAN (IQNA)-Siku kama ya leo miaka 1266 iliyopita, tarehe Mosi tarehe Mosi Dhul Qaadah na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya zenye itibari, alizaliwa Bibi Fatwimat Maasuma SA, binti mtukufu wa Imam Musa al-Kadhim bin Ja'far AS ambaye pia ni mmoja wa Ahlul-Bayti wa Mtume Muhammad SAW.

Alikuwa ni mwanamke mtukufu ambaye katika siku za mwisho za umri wake uliojaa baraka aliaga dunia katika sehemu ya ardhi ya Iran yaani mji wa Qum ambao pia umepambwa kwa ziara lake takatifu.

Sala na salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Mtume Muhammad na Watu wa Nyumba Yake. Sala na Salamu Zimfikie Bibi Fatima Maasuma SA mwanamke azizi ambaye ndugu yake, Imam Ridha AS alisema hivi kuhusu adhama yake:  "Kila ambaye atafanya zaira katika ziara la Maasuma Alayha Salam mjini Qum, ni kama ambaye amenizuru."

Hakuna  shaka kuwa moja ya njia za kuujua Uislamu ni kuijua na kuifahamu sira iliyojaa fahari ya Mtume Muhammad SAW na Watu wa Nyumba yake au Ahul Bayt wake watoharifu. Ingawa katika siku za hivi karibuni maadui wa Uislamu wamezidisha njama na hila zao za kuchafua jina la dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu sambamba na kumvunjia heshima Mtume Mtufuku SAW, lakini ukweli ni kuwa, Uislamu ni dini yenye mafundisho ya kudumu milele na pia sira ya Mtume SAW na Ahul Bayt wake waliotakasika, wote wataendelea kuangazia duni kwa nuru yao isiyozimika. Kwa hakika tunamshukuru Mwenyezi Mungu SWT kutokana na kututunuku neema ya Uislamu, Mtume Muhammad SAW na Ahula Bayt wake. Ni matumaini yetu kuwa Mwenyezi Mungu SWT atupe taufiki ya kuweza kunufaika na maisha yaliyojaa baraka ya Bibi Maasuma SAW.

Fadhila za kielimu

Bibi Maasuma SA alikuwa bintiye Imam Kadhim AS na dada yake Imam Ridha AS na alizaliwa mwaka 173 Hijria Qamaria. Alikuwa na umri wa miaka 10 tu wakati baba yake, Imam Kadhim AS aliuawa shahidi. Kwa msingi huo, zama zake za utotoni zilijawa na majonzi na huzuni ya kuaga dunia baba yake kipenzi. Pamoja na hayo kutokana na kuishi pamoja na ndugu yake aliyetakasika, Imam Ridha AS, cheche za matumaini zilibakia katika maisha yake.  Hadhrat Maasuma SA alikuwa na kiwango cha juu cha imani na utakasifu. Katika zama zake za utotoni alikuwa na fadhila kubwa za kielimu na kimaanawi. Imenukuluwa kuwa, mwamamke huyu mtukufu hata katika zama zake za utotoni alikuwa akijibu maswali mengi sana ya kielimu na kifiqhi.

Wanahistoria wanasema kuwa, Hadhrat Maasuma alikuwa mtaalamu wa Hadithi na pia katika elimu na maarifa alikuwa na daraja la juu. Alijitahidi sana katika kujifunza sayansi na maarifa ya Kiislamu. Hadhrat Maasuma alifikisha amana kwa uaminifu mkubwa kwani kila ambacho alijifunza kutoka kwa baba yake alikifikisha kwa umma pasina kuwepo mapungufu yoyote. Alikuwa akinukulu hadithi kutoka kwa mababu zake na hadithi hizo zilikuwa zikitumiwa na Maulamaa wakubwa Waislamu.

Laqabu ya Sadiqa

Weledi wakubwa wa kidini walimtaja Hadhrat Maasuma kwa lakabu ambayo iliashiria cheo chake cha juu cha kielimu, kimaadili na kimaanawi.  Lakabu kama vile 'Sadiqa' ambayo inamaanisha mwanamke msema kweli sana au lakabu ya  'Muhaditha'  yaani mwanamke  mwenye kufikisha au kusimulia hadithi.  Alikuwa akinukulu hadhiti kutoka kwa baba yake na babu zake watukufu.

Jina la 'Fatima Binti Musa bin Jaafar' limeonekana katika silisila ya baadhi ya riwaya ambapo Maulamaa wa Kishia na Ahli Sunna wamenukulu na kuzikubali riwaya alizoziwasilisha kutokana na kuwa ziliweza kuthibitika na pia zilikuwa sahihi. Kati ya riwaya hizi ni zile zinazonasibishwa na Bibi Fatima Zahra AS na Mtume SAW.  Hadithi hizo ni 'Hadithi ya Ghadir' na 'Hadithi ya Manzilat' kuhusu nafasi ya Imam Ali AS. Katika hadithi hii, Mtume SAW alijinasibisha na Imam Ali AS na kusema nasaba hii ni kama ile ya Harun na Musa (AS).

Hali kadhalika Hadhrat Maasuma SA katika kubainisha tukio muhimu la Ghadir, alifafanua kuhusu hadhi na cheo cha juu cha Ahul Bayt wa Mtume SAW ili watu wasighafilike na kile ambacho waliachiwa na Rasulullah SAW.

Karima wa Ahul Bayt

Kwa mujibu wa riwaya mbali mbali, Hadhrat Maasuma SAW alikuwa na lakabu nyingine mashuhuri ya 'Karima Ahlul Bait'. 'Karima' ni neno lenye maana ya mwanamke mkarimu na mrehemevu. Hadhrat Maasuma SAW alipitisha maisha yake yaliyojaa saada akiwa anajishughulisha na kutoa mafunzi ya Kiislamu na kuifasiri Qur'ani. Aidha alitumia wakati wake wote akijikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kutokana na mwenendo wake huu wa kufuata dini kikamilifu na kutotoka katika mkondo wa uongozi aliweza kufika daraja ya juu ya ukamilifu na ubora wa mwanaadamu. Imam Ridha AS katika kubainisha takuwa ya juu pamoja na utakasifu wa dada yake alimtaja kuwa ni 'Maasuma' yaani mwanamke aliyetakasika na asiyekuwa na dhambi.

Safari ya Imam Ridha ya kubaidishwa kutoka mji wa Madina na kupelekwa Marw nchini Iran mwaka 200 Hijiria, ilifanyika kutokana na sisitizo na vitisho vya Maamun mtawala wa Kiabbasi, na mtukufu huyo alielekea katika mji wa Khorasan nchini Iran pia bila kufuatana na mtu yoyote wa familia yake au watu wa nyumbani kwake. Mwaka mmoja baada ya kuhijiri kaka yake, Bibi Fatima al Maasuma huku akifuatana na baadhi ya kaka zake na watoto wa kaka zake alianza safari ya kuelekea Khorasan kwa ajili ya kumuona kaka yake huyo na muhimu zaidi kutekeleza jukumu la kutetea nafasi ya wilaya na uongozi. 

Alifikisha Ujumbe

Msafara wake ulipokelewa na kulakiwa na watu wengi katika kila mji waliopita. Bibi huyo mtukufu pia alifikisha ujumbe wa kudhulumiwa na kuachwa peke yake kaka yake kwa waumini na Waislamu wa sehemu alizopitia, kama alivyofanya Bibi Zeynab AS, na kuonyesha upinzani wake  na wa Watu wa Nyumba ya Mtume AS dhidi ya utawala uliokuwa umejaa hila wa Bani Abbas. Kwa ajili hiyo, msafara wa bibi huyo mtukufu ulipofika katika mji wa Saveh, baadhi ya watu waliokuwa wakiwapinga Ahlul Bait waliokuwa wakiungwa mkono na vibaraka wa utawala huo waliuzuia msafara huo, na kupigana na waliofutana na bibi huyo suala ambalo lilisababisha karibu wanaume wote wa msafara huo kuuwawa shahidi. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya Bibi Fatima al Maasuma pia alipewa sumu na waovu hao. Alaa Kulli hal Bibi Fatima al Maasuma SA aliugua, labda kutokana na majonzi na huzuni kubwa iliyotokana na tukio hilo au kutokana na athari ya sumu aliyopewa, na kwa kuwa hakuweza tena kuendelea na safari yake kuelekea Khorasan, aliamua kwenda katika mji wa Qum. Alisema: 'Nipelekeni katika mji wa Qum, kwani nilimsikia baba yangu akisema kwamba, mji wa Qum ni kituo cha wafuasi wetu.'

Mji wa Qum

Wakuu wa mji wa Qum walipofahamu kuhusu ujio wake waliharakisha kwenda kumlaki. Mussa bin Khazraj mmoja wa wazee wa mji huo aliwatangulia watu wote kwenda kumlaki bibi huyo mtukufu. Tarehe 23 Rabiul Awwal mwaka 201 Hijiria Bibi Fatima al Maasuma aliwasili katika mji mtukufu wa Qum. Aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubishwa kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW).

Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake  Imam Ridha AS, Bibi Fatima al Maasuma  alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Watu wa Qum na wapenzi wa Ahlul Bait waliuzika mwili wa bibi huyo mtukufu katika eneo ambalo wakati huo lilikuwa nje ya mji lililojulikana kama 'Bustani ya Babol'. Baada ya kuzikwa Mussa bin Khazarj Saibani aliweka juu ya kaburi la mtukufu huyo mikeka mingi. Hali hiyo ilibaki hivyo hadi mwaka 256 Hijiria ambapo Bibi Zeynab binti wa Imam Jawad AS alijenga kuba la kwanza juu ya kaburi la shangazi yake huyo mtukufu, na kwa utaratibu huo eneo hilo alikozikwa mtukufu huyo wa Kiislamu, likawa kivutio cha nyoyo za wapenzi na maashiqi wa Ahlul Bait AS na wafuasi wa Maimamu Watoharifu. Kutokana na baraka ya eneo hilo, hadi hii leo mji wa Qum ni moja ya vituo vikubwa vya elimu ya Ahlul Bait na dini tukufu ya Uislamu.

3730010

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: