IQNA

Magaidi wa Boko Haram wadai kuwateka nyara wanafunzi 300 Nigeria

21:10 - December 16, 2020
Habari ID: 3473462
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram wamedai kuhusika na utekaji nyara wa zaidi ya wanafunzi zaidi ya 300 katika shule moja ya upili Ijumaa iliyopita jimbo la Katsina kaskazini magharibi mwa Nigeria.

“Sisi tumehusika na kilichojiri Katsina,” amesema kinara wa Boko Haram Abubakar Shekau katika  ujumbe wa sauti.

Bashir Salihi Magashi Waziri wa Ulinzi wa Nigeria amefanya ziara huko Katsina kaskazini magharibi mwa nchi hiyo na kuahidi kuwakomboa haraka wanafunzi hao wanaoshikiliwa na magaidi wa Boko Haram.

Itakumbukwa kuwa, Ijumaa 11 Disemba watu wenye silaha waliivamia shule ya sekondari ya serikali ya  katika kijiji cha Kankara huko Katsina na kisha kuwateka nyara wanafunzi kadhaa wa shule hiyo ya upili ya wavulana.  

Gavana wa Jimbo la Katsina la Nigeria Aminu Masari amesema, wapatanishi wa mazungumzo wa serikali wanawasiliana na wateka nyara wa wanafunzi  hao.

Hii si mara ya kwanza magaidi wa Boko Haram kuwateka wanafunzi nyara kutoka shuleni.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa, ambayo inatumiwa na aghalabu ya Waislamu wa Nigeria, lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Halikadhalika ugaidi huo wa Boko Haram umepelekea Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria kubakia nyuma kimaendeleo na hivyo kuathiri vibaya mustakabali wao. Serikali ya Nigeria pia inalaumiwa kwa kuzembea katika kukabiliana na magaidi hao huku kukiwa na ripoti kuwa baadhi ya majenerali jeshini na maafisa wa serikali wanaofaidika na ugaidi huo wa Boko Haram.

3473414

captcha