IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu uko Niger kwa upatanishi

21:04 - August 13, 2023
Habari ID: 3477431
TEHRAN (IQNA)- Viongozi wa Kiislamu kutoka Nigeria wamewasili nchi jirani Niger pamoja ikiwa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kurejesha amani katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.

Vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti kwamba Sheikh Abdullahi Bala Lau ameongoza ujumbe wa Maulamaa wa Kiislamu kufuatia idhini iliyotolewa kwa maulamaa na Rais Bola Tinubu wa Nigeria kuingilia kati na kujadiliana na wenzao wa Jamhuri ya Niger.

Sheikh Lau na timu yake waliwasili Niger siku ya Jumamosi na kukaribishwa na wanazuoni wa Kiislamu katika nchi hii.

Baada ya kukutana na Sheikh Lau, kiongozi wa mapinduzi ya Niger yuko tayari kufikiria suluhu la kidiplomasia kwa mzozo uliopo kati ya nchi yake na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambayo imetishia kuingilia kijeshi kuwarejesha madarakani watawala wa kiraia waliopinduliwa.

Jenerali Abdourahamane Tiani "alisema milango yao iko wazi kuchunguza diplomasia na amani katika kutatua suala hilo," msomi huyo alisema katika taarifa baada ya ujumbe wake kufanya mazungumzo katika mji mkuu wa Niamey wa Niger.

Rais Tinubu wa Nigeria siku ya Jumatano alikutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu nchini humo ambao waliomba kibali chake ili kuingilia kati na kujadiliana na wenzao nchini Niger.

Wanazuoni wa Kiislamu wanapinga pendekezo la Jumuiya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS la kuingilia kijeshi mgogoro wa Niger na kubaini kuwa mbali na athari mbaya za migogoro ya silaha, wameamrishwa na imani yao ya kidini na Qur'ani Tukufu kutafuta usuluhishi kwanza katika kesi kama hizi kabla ya kuanza vita.

Ikumbukwe kuwa,  tarehe 26 mwezi uliopita wa Julai, wanajeshi wa Niger walimpindua Rais Mohamed Bazoum na wanamshikilia hadi hivi sasa. Jeshi likiongozwa na Abdourahmane Tchiani sasa linashikilia madaraka Niger.

Nchi za Magharibi hasa Marekani na Ufaransa zimepata pigo kutokana na kupinduliwa Bazoum ambaye wananchi wa Niger wanasema alikuwa kibaraka mkubwa wa madola ya Magharibi.

Licha ya Niger kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili kama uranium, lakini imeendelea moja ya nchi maskini zaidi duniani huku utajiri huo ukikombwa na madola ya Magharibi hasa Ufaransa. 

Tayari utawala wa kijeshi nchini Niger umetangaza serikali mpya ya mpito na kumteua Ali Lamine Zeine kuwa waziri mkuu wa muda na Baraza la Mawaziri lenye watu 21. Hiyo ni hatua kubwa muhimu iliyochukuliwa nchini Niger baada ya mapinduzi ya kijeshi.

4162090

 

Kishikizo: niger nigeria waislamu
captcha