IQNA

Utawala ghasibu wa Israel watakiwa uwape Wapalestina chanjo ya corona

22:09 - January 15, 2021
Habari ID: 3473559
TEHRAN (IQNA)- Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema utawala wa Israel, kama utawala vamizi unaokali ardhi za Palestina kwa mabavu, unapaswa kuwapa Wapalestina chanjo ya corona.

Wataalamu hao wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wametoa taarifa wakiitaka Israel itekeleze majukumu yake ya kisheria ya kuhakikisha Wapalestina wanapata haraka chanjo ya corona.

Halikadhalika wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamebainisha wasiwasi wao kufuatia hatua ya wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kutowapa chanjo ya corona Wapalestina.

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unakataa kuwapatia chanjo ya corona mateka Wapalestina unaowashikilia kwenye magereza yake.

Idara ya habari inayohusika na masuala ya mateka Wapalestina imetangaza kuwa, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni anashikilia kwamba, mateka Wapalestina wa masuala ya usalama wasipigwe chanjo ya corona na kwamba chanjo hiyo itolewe kwa wafanyakazi tu wa magereza wanakoshikiliwa Wapalestina hao, uamuzi ambao unahalifu taratibu na hati za kimataifa.

Idara hiyo ya habari inayohusika na masuala ya mateka Wapalestina imetahadharisha kuhusu hatari inayowakabili mateka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, kubainika kesi nyingine mpya za watu walioambukizwa virusi vya corona katika kitengo cha nne cha jela ya Raymun kunaashiria hatari kubwa sana inayowakabili mateka hao.

3947821

Kishikizo: Corona palestina israel
captcha