IQNA

Uafriti wa Israel wa kutaka kuvuruga uchaguzi wa Palestina

20:46 - March 23, 2021
Habari ID: 3473755
TEHRAN (IQNA) -Mkuu wa shirika la usalama wa ndani la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Shin Bet amemtaka Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aghairishe uchaguzi wa Palestina ikiwa harakati ya Hamas itashiriki katika uchaguzi huo.

Baada ya kupita miaka 15, Wapalestina wanataraji kuona uchaguzi unafanyika katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu. Uchaguzi wa bunge umepangwa kufanyika tarehe 22 Mei, uchaguzi wa rais tarehe 31 Julai na ule wa baraza la taifa la Palestina unatazamiwa kufanyika tarehe 31 Agosti ya mwaka huu wa 2021.

Uchaguzi wa mwisho wa Palestina ulifanyika mwaka 2006. Katika uchaguzi huo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS iliibuka mshindi kwa kujipatia viti 75 kati ya viti vyote 132 vya bunge. Baada ya uchaguzi huo, Ismali Hania aliunda baraza la mawaziri la Palestina. Tukio hilo lilikuwa na matokeo mawili muhimu. Matokeo ya kwanza ni kwamba, kutokana na ushindi huo iliopata Hamas Umoja wa Ulaya na Marekani zilikataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi na zikatangaza kuwa hazitatoa mashirikiano kwa serikali iliyoundwa na Hamas; na kwa kisingizio cha kuitambua kuwa ni harakati ya kigaidi, iliiwekea vikwazo pia harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina. Lakini matokeo mengine ni kwamba, vita vya ndani vilizuka baina ya Wapalestina; na hatimaye serikali iliyoundwa na Hania ilisambaratika na tofauti za ndani baina ya Palestina ya Ufukwe wa Magharibi na ya Ukanda wa Gaza zikashtadi na zingalipo mpaka sasa hivi.

Uafriti wa Israel wa kutaka kuvuruga uchaguzi wa Palestina

Hivi sasa, na baada ya miaka 15, uchaguzi umepangwa kufanyika huko Palestina huku tathmini za hivi karibuni kabisa zikionyesha kuwa harakati ya Hamas ina nafasi kubwa ya kuibuka mshindi, jambo ambalo limeutia wasiwasi utawala wa Kizayuni na kuufanya utoe onyo na indhari kwa Mahmoud Abbas ambaye ni rais wa Mamlaka ya Ndani na kiongozi wa harakati ya Fat-h.

Uafriti wa Israel wa kutaka kuvuruga uchaguzi wa Palestina

Utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel una makubaliano ya kiusalama na mashirikiano kadhaa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, ambapo kwa kuzingatia uadui mkubwa uliopo kati ya utawala huo na Hamas, makubaliano na mashirikiano hayo hayatodumu ikiwa Hamas itapata ushindi katika uchaguzi wa Palestina. Kamil Abu Rukun, mratibu wa utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina ya Ufukwe wa Magharibi yanayokaliwa kwa mabavu ametangaza kuwa, Israel haitaweza katu kuendelea kuheshimu mikataba iliyosaini, ikiwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina itakuwa chini ya uongozi wa Hamas. Aidha amesisitiza kwa kusema, "endapo Hamas itashinda uchaguzi ushirikiano wa kiusalama hautakuwa na maana tena na itabidi tujiulize, mikataba tuliyosaini itakuwa na thamani na itibari gani tena?"

Kwa kutilia maanani uwezekano huo wa Hamas kushinda katika uchaguzi wa Palestina, Nadav Argaman mkuu wa shirika la usalama wa ndani la utawala wa Kizayuni wa Israel Shin Bet, ambaye kwa mujibu ya tovuti ya habari ya The Times of Israel wiki mbili zilizopita alisafiri kuelekea mjini Ramallah, amemtaka Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aghairishe uchaguzi huo wa Palestina ikiwa Hamas itashiriki pia. Amos Harel, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa gazeti la Haaretz ameeleza kwenye makala aliyoandika katika gazeti hilo kuwa, "Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mpaka sasa hajazipa umuhimu indhari zilizotolewa na Israel kuhusu uwezekano wa Hamas kupata ushindi na kuyadhibiti maeneo mengi ya Ufukwe wa Magharibi."

Uafriti wa Israel wa kutaka kuvuruga uchaguzi wa Palestina

Indhari na kauli hizo za hofu na wasiwasi zinaonyesha kuwa, Israel ambayo yenyewe, leo itakuwa na uchaguzi wa nne wa bunge unaofanyika ndani ya kipindi cha miaka miwili huko katika ardhi hizo unazozikalia kwa mabavu, imeamua kuendeleza uafriti wa kutaka kukwamisha na kuvuruga uchaguzi wa Palestina. Kuhusiana na suala hilo, Husam Badran, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema: "Utawala ghasibu ndio upande wa kwanza na mkubwa zaidi unaonufaika na mpasuko unaotokea baina ya makundi ya Palestina; na unazichukulia kuwa tishio halisi kwake jitihada zozote zinazofanywa kwa ajili ya kuziba mpasuko baina ya makundi ya Palestina; na wala hautaki sisi tujitokeze mbele ya dunia katika hali ya taifa moja lililostaarabika".

parstoday.com/sw

 

captcha